'Wimbo gani' haijaingiza hata shilingi hadi sasa

Muktasari:

"Huwezi amini wimbo huu bado haujatuingizia chochote licha ya mashabiki wengi kuumiliki, una wiki mbili  sasa tangu upikwe studio, bado mfumo wa urasimishwaji unatakiwa uzingatiwe zaidi ili wasanii tunufaike na kazi zetu," alisema Diamond.

'Muziki Gani' wimbo ulioimbwa na Naseeb Abdul 'Diamond' pamoja na Nay wa Mitego uliojipatia umaarufu mkubwa tangu kutolewa wiki mbili zilizopita, umeshaenea kwa Watanzania wengi huku wasanii hao wakidai kuwa hawajapata hata shilingi 100 kupitia wimbo huo.

Wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti wasanii hao walisema wimbo huo ulijizoelea umaarufu mkubwa huku mashabiki wakipakua muziki huo kwa kasi kupitia mitandao na blogu mbalimbali.

"Huwezi amini wimbo huu bado haujatuingizia chochote licha ya mashabiki wengi kuumiliki, una wiki mbili  sasa tangu upikwe studio, bado mfumo wa urasimishwaji unatakiwa uzingatiwe zaidi ili wasanii tunufaike na kazi zetu," alisema Diamond.

Diamond alisema wao kama wasanii waliamua kuuachia wimbo huo kutokana na kushindwa kuuhifadhi kwa kuwa bado mfumo wa ununuzi wa nyimbo kupitia vyombo hivi haujawa imara.

Nay wa Mitego alisema licha ya kazi kadhaa alizowahi kufanya na Diamond, wimbo huu umekuwa bora zaidi na kupendwa na mashabiki, ingawaje wapo wasanii wenzake wa Hiphop wanamponda.

Rapa wa Tanzania aishiye nchini Marekani, Wakaza aliuponda wimbo huo na kuuita ni wimbo wa kipumbavu, suala ambalo lilipokelewa  tofauti na mashabiki wa Diamond.