Wednesday, April 3, 2013

Q Chief awaza bendi!

 

By Benny Felix, Mwananchi

Msanii wa muda mrefu katika muziki wa kizazi kipya, Abubakar  shaaban Katwila, maarufu kama Q Chief au Q Chillah kama wengi walivyozoea kumuita, ambaye alikuwa kimya kwenye muziki kwa muda mrefu, ameeleza azma yake ya kurudi kupiga muziki wa bendi.


Mawazo yake hayo yamekuja baada ya uzinduzi wa wimbo wake mpya ynaoendelea kusikika katika vituo mbali mbali vya redio ambao aliuzindua siku za karibuni katika ukumbi wa Maisha Club.


Katika maongezi yake na Mwananchi, Mwanamuziki huyo ambaye amewahi kutamba na vibao kama Aseme, Ninachokipata, U Hali gani, na nyingine, amesema huwa anajisikia kuwa mwanamuziki hasa, anapofanya kazi na bendi, lakini anapofanya kazi na muiziki wa Dj huhisi kuna kitu kimepotea.


Q Chief aliwahi kufanya uzinduzi wa bendi yake iliyojulikana kwa jina la Atomic, ambayo ilifanya maonesho machache kabla ya kupotea kwenye tasnia miaka mitano iliyopita, lakini bendi hiyo haikuweza kukaa kwa muda mrefu na kufanya vizuri kama Machozi Band, B Band au Top Band ambazo zinamilikiwa na wasanii wa kizazi kipya pia.


“Msanii wa ukweli ili aweze kukamilika lazima aweze kuimba na band au kumiliki bendi kabisa. Unaweza kuona hata wasanii maarufu duniani siku hizi hawaimbi na playback, kwa hiyo kama Q Chillah mpya nipo katika mpango wa kuirudisha bendi yangu na wanamuziki wapya kabisa.


Tunakaa na wadau kuzungumzia ili swala la bendi na pia inaweza isirudi kwa jina lile lile la Atomic".


Lakini wapenzi wa kazi zangu wajue kwamba bendi ya Q Chillah inakuja, pia nina nyimbo nyingi za kutosha kupata kiota kimoja nitoe burudani siku za weekend kwa wapenzi wa muziki wangu”, alibainisha Q Chief

-->