VIDEO-Ali Kiba alivyoitumia harusi yake kibiashara

Muktasari:

  • Shamrashamra zilianza Aprili 19 pale mjini Mombasa, Kenya ambapo asubuhi ya saa 12, Ali Kiba alifunga ndoa na Amina Khaleef katika msikiti wa Ummul Kulthum. Amina ni mwenyeji wa Mombasa.Jioni ilifuatia sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Mombasa na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Gavana wa jimbo hilo, Hassan Joho, ambaye ni rafiki wa karibu na Ali Kiba.

Aprili umekuwa mwezi wa faraja kwa familia ya Salehe Kiba baada ya vijana wao wasanii wa Bongo Fleva, Abdu Kiba na Ali Kiba kufunga ndoa.

Shamrashamra zilianza Aprili 19 pale mjini Mombasa, Kenya ambapo asubuhi ya saa 12, Ali Kiba alifunga ndoa na Amina Khaleef katika msikiti wa Ummul Kulthum. Amina ni mwenyeji wa Mombasa.Jioni ilifuatia sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Mombasa na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Gavana wa jimbo hilo, Hassan Joho, ambaye ni rafiki wa karibu na Ali Kiba.

Sherehe zikaendelea kuiandama familia hiyo kwani jijini Dar es Salaam, mdogo wa Ali Kiba, Abdu Kiba alifunga ndoa na Ruwayda Aprili 22. Baada ya Abdu na Ali kufunga ndoa, Aprili 29, sherehe ya pamoja ilifanyika ambayo kila mtu alikuwa akisubiri kwa hamu kuona tofauti na yale yaliyotokea Mombasa ukizingatia kuwa hapa ndio nyumbani kwao.

Sherehe hiyo ilifanyika katika hoteli ya nyota tano ya Serena iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam, ilianza saa 1.30 usiku na kuhitimishwa saa 6.10 usiku.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo mke wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, mama Salma Kikwete, ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa. Wengine waliokuwepo ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Ally Mwalimu, Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete.

Kwa upande wa wasanii alikuwapo Mwana FA, Christian Bella, Vanessa Mdee, MimiMars, Idris Sultan, Bilnass, Eshe Buheti, Ommy Dimpoz ambaye alikuwa mwanakamati na wengine wengi.

Wadau wa mpira pia hawakuwa nyuma, Haji Manara Msemaji wa klabu ya Simba alinogesha sherehe hizo na wachezaji Emmanuel Okwi na Nadir Haroub Canavaro.

Kulipwa kuirusha kwenye TV

Pamoja na matukio mbalimbali kufanyika katika sherehe hizo, kikubwa na ambacho hakitasahaulika kwa Kiba ni kutumia nafasi hiyo kufanya biashara.

Moja ya biashara hiyo ni kulipwa pesa ndefu na kituo cha televisheni cha Azam, ambacho kilikuwa kikirusha matangazo ya shughuli hiyo moja kwa moja kuanzia sherehe za Mombasa na Dar es Salaam.

Tukio hilo halijawahi kufanyika hapa nchini hususani kwa wasanii ambao wameshawahi kufunga ndoa.

Kwa mujibu wa meneja wake, Christina Mosha ‘Seven’, baada ya harusi hiyo kuzua gumzo mjini Mombasa, baadhi ya kampuni zikiwemo za mitandao ya simu zilijitokeza kutaka kuibeba shughuli hiyo. Hata hivyo, anasema ilikuwa ngumu kuwakubalia kwa kuwa Azam tayari walikuwa wamewahi kuichukua kwa sehemu zote yaani Mombasa na Tanzania.

Hivyo ukiangalia hapo, huenda Kiba hela ya michango hakuihitaji kama ambavyo shughuli nyingine za harusi zimekuwa zikifanyika kwa watu kuchangsihana, Kiba yeye amelipwa. Pia, kitendo hicho kitamfanya ale fungate yake kwa raha bila kuwaza madeni ya shughuli nzima.

Kuzindua kinywaji

Tukio jingine kubwa lililojitokeza katika harusi hiyo ni ile ya kuzindua kinywaji chake cha kuongeza nguvu alichokipa jina la Mofaya.

Kinywaji hicho alikitambulisha baada ya waalikwa kumaliza kupata chakula cha jioni na kueleza nia yake ya kuingia katika biashara hiyo.

Katika maelezo yake anasema kupitia mashabiki wake kumsikiliza na kumwangalia ameweza kuwekeza katika sekta nyingine.

Anasema kama ameweza kwenye muziki aliona hata kwingine inawezekana kwani watu wamemzoea kumuona kwenye tasnia ya muziki, lakini ameona kupitia umaarufu alionao si mbaya kuwekeza.

Ali Kiba ameitumia vyema harusi yake. Kwanza kwa kuzindua kinywaji wakati wa sherehe maana yake ujumbe umekwenda mbali. Wale waliokuwapo ukumbini na watazamaji wa Azam waliokuwa wameganda kwenye televisheni zao usiku. Hivyo kwa matukio hayo mawili makubwa utaona ni namna gani Ali Kiba ameweza kutumia sherehe za harusi yake kuingiza hela badala ya kuteketeza fedha.

Maoni ya wasanii na waalikwa

Naye mtangazaji na mwandishi wa habari maarufu, Millard Ayo, amesema harusi ya msanii Ali Kiba na Ambwene Yessayah’AY’ zimemshangaza kutokana na kuwepo kwa usiri wake. Hata hivyo pamoja na hilo, aliwashauri wengine ambao wapo katika mpango huo wasiingie kwa kukurupuka kwa lengo la kupostiwa kwenye mitandao kama ilivyokuwa kwa wasanii hao kwa madai wanaweza kuja kujutia baadaye.

Ayo alisema kwa upande wa ndoa ya Ali Kiba pamoja na kuwa mtu wake wa karibu, aliijua wiki mbili kabla ya kufanyika.

Wakati kwa AY alisema hilo ndilo jambo ambalo hakulitarajia kabisa, kwani amekuwa ni mtu wa kufanya mambo yake kwa siri tofauti na wasanii wengine ambao wakiwa na tukio la aina hiyo utaona hata dalili.

Alipoulizwa ni lini na yeye watu watarajie kumuona akioa, alisema “Unajua ndoa si jambo dogo linahitaji kujitafakari na ninawashauri na wengine wanaotaka kufanya hivyo wasitake kuiga kisa tu wamewaona kina Kiba na AY ili kupata watazamaji kwenye mitandao ya kijamii,” alisema.

Naye msanii Bilnas alisema kwake harusi hiyo imezidi kumchanganya zaidi baada ya kuona Kiba ameweza kuoa wazazi wake wote wakiwa bado wapo hai, jambo ambalo ni la kumshukuru Mwenyezi Mungu.

“Kiukweli hii harusi wengi imetuchanganya na kutuamsha kuwa ukitaka kufanya jambo kama hili inawezekana tena inakuwa vizuri na wazazi wakalishuhudia kama alivyofanya mwenzetu Kiba.

“Amenitamanisha kiukweli na mimi niingie katika kundi la wanandoa, na ninaahidi nitafanya hivyo muda si mrefu,” alisema Bilnas mkali wa kibao cha Mazoea.

Kwa upande wake Christian Bella, alisema harusi ya Kiba imempa fundisho naye sasa kuangalia namna ya kuanza kutoka kwenye maisha ya ‘ubachela’.

“Unajua si jambo dogo kwa msanii kijana kuamua kuoa akiwa katika umri mdogo, tunapitia vishawishi vingi ambavyo kama hutakuwa makini unaweza ukajikuta kila siku hutaki kuitwa mume wa mtu,” alisema Bella.

Naye msanii Mimi Mars, alisema kwamba hatua ya wasanii wa Tanzania iliyofikiwa kwa kutambuliwa umuhimu wao ni nzuri ikiwemo hiyo ya Ali Kiba harusi yake kuonyeshwa mubashara.

Mars alisema mbali ya Kiba kuingiza fedha harusi hiyo pia imewadhirishia Watanzania na watu wengine waliokuwa wakifuatilia harusi hiyo kuwa wasanii ni watu wa kawaida kama walivyo watu wengine ambapo ikifika muda wa kuoa na kuolewa nao hufanya hivyo.