Pombe ya viroba yapigwa marufuku Afrika nzima

January Makamba-Waziri wa Nchi, Ofisi ya M/Rais, Muungano na Mazingira

Muktasari:

Wakati zikiwa zimesalia siku tano kabla ya kuanza kutekelezwa kwa amri hiyo, nchini Malawi sakata hilo limekuwa ni vita kati ya “afya na biashara”.

Dar es Salaam.Moto uliowashwa na Serikali, kuzuia kuuzwa kwa pombe kali zinazowekwa kwenye mifuko midogo ya plastiki, maarufu viroba umetapakaa barani Afrika.

Wakati zikiwa zimesalia siku tano kabla ya kuanza kutekelezwa kwa amri hiyo, nchini Malawi sakata hilo limekuwa ni vita kati ya “afya na biashara”.

“Pombe ina madhara hasi katika ubora wa mfumo wa elimu,” alisema Mkuu wa   Sekondari ya Livuzu ya Blantyre, P. Simbota alipozungumza na gazeti la Nyasa Times.

“Pakiti hizi zina kiwango kikubwa cha kilevi na zinauzwa kwa bei ndogo. Wanafunzi hunyonya wakati wa masomo, kwa kuwa ni ndogo na rahisi kuzificha. Wengine huchanganya hata na maji ya kawaida au juisi na hivyo kuficha tabia zao hatarishi.”

Tayari, Serikali nchini imepiga marufuku pombe hizo, ambazo nyingi huwa na kiwango cha kilevi kinachofikia kati ya asilimia 30 na 40, kwa maelezo kuwa zinachafua mazingira, ni rahisi kutumiwa na vijana wadogo na hata watoto wa shule za msingi.