Jela miaka 30 kwa kumbaka ‘bubu’ mlemavu wa akili

Muktasari:

  • Mwendesha mashtaka alidai baada ya mlemavu huyo kufanyiwa kitendo hicho alitoka nje na kuwaonyesha ishara watu kuwa amebakwa.

Katavi. Mahakama ya wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemuhukumu Ramadhani Shaban (24) mkazi wa mtaa wa Majengo B kifungo cha miaka 30 jela baada  ya kumpata na hatia ya kumbaka mtu mwenye ulemavu wa kuongea ‘Bubu’ na akili mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa).

Hukumu ya kesi hiyo iliyovuta hisia za  watu wengi wa mjini Mpanda imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya  Mpanda, Gasper Luoga baada ya mshitakiwa kukiri kutenda kosa hilo.

Awali  katika hati mashtaka,  mwendesha mashtaka ambaye ni mwanasheria wa Serikali mkoa wa Katavi, Flaviana Shio alidai mahakamani hapo kuwa, Shabani  alitenda kosa hilo Septemba 9 saa 12:00 jioni katika mtaa wa Majengo B.

Alidai siku yatukio mshitakiwa  alikwenda kwenye maeneo ya mtaa wa  Mji  Mwema alikokuwa akiishi mlalamikaji kwa mjomba wake Ernest Chambala na kumpakia kwenye baiskeli yake.

Alidai baada ya kumpakia alikwenda naye hadi kwenye chumba chake alichopanga katika mtaa wa Majengo B na kisha alianza kumbaka mpaka alipomaliza haja yake.

Mwendesha mashtaka huyo alidai baada ya mshitakiwa kumaliza kitendo hicho, mlemavu huyo wa kuongea na akili  alitoka nje na kuanza kuwaonyesha watu ishara kuwa amebakwa.
  
Alidai mjomba  wa mlalamikaji huyo alianza kumsaka mtu aliyehusika kutenda kitendo cha kumbaka mpwa wake ambaye alimwongoza  hadi  kwenye  nyumba na chumba alichofanyiwa kitendo hicho kibaya.

Alidai majirani wa nyumba hiyo walipoulizwa kama walimwona mlemavu huyo akiingizwa kwenye chumba cha mshitakiwa walithibitisha kumwona akiingia naye ndani.

Mshitakiwa  baada ya  kukamatwa   alichukiliwa  na  kupelekwa kituo cha polisi cha Mpanda na katika maelezo yake alikiri kutenda kosa la  kumbaka mlemavu huyo na taarifa za daktari zilionyesha alikuwa ameingiliwa na  mwanaume.

Baada ya mshitakiwa kukiri kosa, Hakimu Luoga alimweleza Mahakama imemtia hatiani hivyo kama anayo sababu yoyote ya msingi ya kuishawishi mahakama impunguzie adhabu    anapewa nafasi ya kujitetea .

Katika utetezi wake aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa mama yake mzazi anamtegemea kwani baba  yake ameishafarikidunia.

Hakimu Luoga baada ya kusikiliza  utetezi huo, aliiambia  Mahakama  kuwa  mshitakiwa amepatikana  na  hatia kwa mujibu wa kifungu cha sheria  Namba  130 (1)  (2) e na  131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Hivyo, alimuhukumu Shabani kwenda kutumikia  jela  kifungo cha miaka 30.