Kesi za wabunge Chadema zinavyotia doa siasa za ushindani

Viongozi wa Chadema  wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe wakimsikiliza mwanasheria wao, Peter Kibatala (kulia) wakati wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Ndiyo. Wapalestina wamekuwa wakishuhudia wabunge wao wengi wakifungwa jela kwa wakati mmoja kuliko sehemu yoyote duniani.

Je, Tanzania inataka kufanana na Palestina? Kwa hali halisi kisiasa, haiwezi kutengeneza sura yenye kufanana na nchi hiyo.

Ndiyo. Wapalestina wamekuwa wakishuhudia wabunge wao wengi wakifungwa jela kwa wakati mmoja kuliko sehemu yoyote duniani.

Mpaka mwaka 2015 unamalizika, wabunge 12 wa nchi hiyo walikuwa jela, wengine kwa kuhukumiwa baada ya kukutwa na hatia na wengine walishikiliwa kwa nguvu za kijeshi na kuwekwa kizuizini pasipo hatua za kisheria kuchukuliwa.

Tanzania haiwezi kuwa sawa na Palestina kwa sababu wabunge wa nchi hiyo wanakamatwa, wanashtakiwa na kufungwa katika nchi jirani ya Israel. Hata wale ambao mashtaka yao hayaendi mbele ya sheria, nao wanawekwa kizuizini hukohuko ugenini.

Haiwezekani kwa Tanzania kufikisha wabunge 12 jela kwa wakati mmoja kama Palestina, ila kuwa na mfungwa mmoja mbunge ni aibu, kwa sababu yanayowatokea yanafanyika hapa nchini, wakati Wapalestina wanatendewa hayo na nchi jirani ya Israel.

Wabunge wafuatao wa Palestina; Khalida Jarrar, Aziz Duwaik, Marwan Barghouti, Ahmad Sa’adat, Hassan Yousef, Mohammad Jamal Al-Natsheh, Muhammad Bader, Azzam Shalhab, Nayef Rajoub, Hosni Al-Burini, Riyadh Raddad na Muhammad Abu Tir, mwaka 2015 walikuwa jela kwa wakati mmoja nchini Israel.

Siasa za Palestina na Israel zinafahamika. Kwa hiyo mbunge wa Palestina akiwekwa jela Israel huchukuliwa kama shujaa anayepigania taifa huru la Palestina. Sawa na Tanzania ingekuwa na mgogoro wa mipaka na nchi yoyote jirani, halafu mbunge wa Tanzania ashikiliwe na hiyo nchi, huyo ataitwa shujaa.

Tanzania mbunge kufungwa jela si ushujaa ni aibu kwa mbunge mwenyewe ikiwa kuna makosa dhahiri ya mbunge. Aibu hiyo inakwenda kwenye jimbo lake na taifa kwa jumla. Inapotokea mbunge anafungwa kwa uonevu, hiyo ni taathira kwa mfumo wa mamlaka za nchi.

Alama ya kuuliza hutambaa kichwani kuhusu jinsi dola inavyofanya kazi zake kwa kufuatisha mgawanyo wa mamlaka ya mihili yake. Mbunge kufungwa au kuandamwa na kesi za jinai, ni ama kielelezo cha mhimili wa Bunge kutoheshimika au kukosekana kwa ustaarabu wa kisiasa baina ya wanasiasa.

Tafsiri ya mhimili wa Bunge kutoheshimika ina matawi mawili; mosi, ni mbunge mwenyewe kutojiheshimu, kutoheshimu chombo anachokitumikia pamoja na dhima ambayo anakuwa ameibeba kutoka kwa wananchi anaowawakilisha kisha kutenda makosa ya jinai kiholela. Pili ni Serikali kutoheshimu Bunge, hivyo kutojali hadhi ya mbunge, kisha kumfungulia mashtaka kwa uonevu au kwa makosa yenye kuhitaji subira na kuvumiliana.

Kesi wabunge Chadema

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye ni mbunge Hai, vilevile Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam. Mashtaka ya Mbowe ni kuchochea ghasia, kukaidi amri ya polisi na uasi.

Katika kesi hiyo, Mbowe anashtakiwa pamoja na wabunge sita; John Mnyika (Kibamba), Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Esther Matiko (Tarime Vijijini) na Halima Mdee wa Kawe. Kwa pamoja wanashtakiwa kwa makosa 12 ya uchochezi, ukaidi na uasi.

Wabunge hao wanatuhumiwa kufanya uchochezi, ukaidi na uasi huo Februari 16, mwaka huu, wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wanakwenda kwa msimamizi wa uchaguzi Kinondoni kufuatilia viapo na utambulisho wa mawakala.

Tukio hilo lililosababisha polisi wawatawanye viongozi na wafuasi hao. Matumizi ya nguvu yalichukua nafasi hadi risasi za moto zilitumika.

Kuna viongozi wengine wa Chadema wapo kwenye orodha hiyo; Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye ndiye alikuwa mgombea ubunge wa Kinondoni katika uchaguzi mdogo. Hata hivyo, katika uchambuzi nawalenga zaidi wabunge wenye kesi, kwani wana majukumu makubwa wamebeba lakini wanalazimika kutumia muda mwingi kuhudhuria kesi mahakamani.

Faili la kesi kubwa

Mbowe na wabunge wengine sita jumla ni saba. Mbunge wa nane mwenye kesi ni Paschal Haonga (Mbozi), anayeshtakiwa kwa kufanya fujo na kuvuruga katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Mji mdogo wa Mlowo. Kwamba Agosti 28, mwaka jana, Haonga akiwa na wenzake wawili, waliwazuia polisi kufanya kazi yao.

Katika kesi hiyo, watu wengine wawili wanaoshtakiwa pamoja na Haonga ni Wilfred Mwalusanya ambaye ni katibu wa mbunge (Haonga) na Mashaka Mwampashi. Hukumu yao ilikuwa isomwe Julai 10, mwaka huu lakini iliahirishwa mpaka Agosti 10, mwaka huu, baada ya Hakimu Mkazi Wilaya Mbozi, Nemes Chami kueleza kwamba hukumu ilikuwa haijakamilika.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alitoka jela Mei mwaka huu. Alikuwa akishikiliwa kwenye gereza la Ruanda, Mbeya, baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kutoa maneno yenye kumvunjia heshima Rais John Magufuli. Sugu alihukumiwa kwenda jela miezi mitano, ingawa aliachiwa kabla ya muda.

Sugu ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa muziki wa kizazi kipya, baada ya kutoka jela alitoa wimbo wenye jina 219 ambayo ni namba yake ya mfungwa gerezani. Ndani ya wimbo huo, Sugu anajitambulisha kama mfungwa wa kisiasa na kwamba alitiwa hatiani bila kosa. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeufungia wimbo huo na Sugu ameahidi kuipeleka Basata mahakamani.

Unapomwongeza Sugu kwenye orodha ya faili la kesi za wabunge Chadema, jumla anakuwa wa tisa, wa kumi ni mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali ambaye Januari mwaka jana, alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kufanya fujo kwenye uchaguzi wa baraza la madiwani, Halmashauri ya Kilombero, baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.

Lijualikali alikaa jela kwa miezi mitatu kabla hukumu iliyomweka jela ya Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, kutenguliwa na Mahakama Kuu Machi mwaka jana. Lijualikali alikutwa na hatia pamoja na dereva wake ambaye alifungwa kifungo cha nje. Mahakama Kuu ilipotengua hukumu ya awali, wote wawili waliachiwa huru.

Vilevile, Lijualikali ana kesi nyingine pamoja na mbunge mwenzake wa Mlimba, Suzan Kiwanga wakidaiwa kuchoma moto ofisi ya mtendaji.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alikula Krismasi ya mwaka 2016 kisha kuanza mwaka 2017 akiwa mahabusu ambako alikuwa akishikiliwa baada ya kunyimwa dhamana kwa takriban miezi minne. Baadaye uamuzi wa Mahakama Kuu, ulitolewa kueleza kwamba hakukuwa na sababu yoyote ya msingi ya kumnyima dhamana. Kesi hiyo bado inaendelea. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kipindi hiki akiendelea na matibabu Brussels, Ubelgiji, ni kama pia anapumua na hekaheka za polisi, mahabusu na mahakamani, kwani kabla ya Septemba 7, mwaka jana, alikuwa na rekodi ya kuwa mbunge wa Chadema na upinzani kwa jumla mwenye kupatikana sana polisi, mahabusu na mahakamani kwa kushtakiwa.

Septemba 7, mwaka jana, Lissu ambaye ni wakili maarufu, vilevile mwanasheria mkuu wa Chadema, alipigwa risasi akiwa kwenye gari, kabla hajashuka nyumbani kwake baada ya kutoa bungeni.

Halima ana kesi nyingine inayoendelea Kisutu, Dar es Salaam, akituhumiwa kutoa maneno ya kuudhi dhidi ya Rais Magufuli. Ukiweka idadi yote pamoja; Mbowe, Lissu, Halima, Sugu, Lijualikali, Haonga, Mnyika, Bulaya, Matiko, Heche, Sugu na Lema jumla ni 12 ambayo ni idadi sawa na wabunge 12 wa Palestina walioshikiliwa na Israel mwaka 2015.

Pamoja na ukweli kuwa wabunge 12 wa Chadema hawajashikiliwa kwa wakati mmoja, lakini upo ukweli usiojificha kwamba wabunge hao na wengine wa upinzani wamekuwa wakipishana mahabusu katika maeneo mbalimbali ya nchi. Jambo ambalo halivutii kabisa ni kuona kwamba kesi zinakuwa nyingi mpaka zinaingilia muda wao wa kutumikia wananchi.

Mathalan, Mbowe, Matiko, Bulaya, Msigwa na Heche ni wabunge wa majimbo ya mikoa ya mbali na Dar es Salaam. Hata hivyo, kutokana na kukabiliwa na mashtaka, hulazimika kuacha shughuli za majimbo yao au hata kutoroka bungeni ili waweze kuhudhuria mahakamani Kisutu, Dar es Salaam.

Hali hiyo inawaumiza sana wananchi wa majimbo wanayoyawakilisha, maana kuna huduma mbunge hawezi kutoa. Athari pia ipo kwa Bunge, kwani wajumbe wake hushindwa kutekeleza majukumu ya kibunge kama inavyotakiwa ili wapate mwanya wa kufika mahakamani.

Utaona kwamba yapo mambo mengi yenye faida hukosa kutekelezwa na wabunge wenye kesi kwa sababu upatikanaji wao bungeni na majimboni unakuwa wa taabu kutokana na kubanwa na kesi.

Jambo lisilostahili kusahaulika ni kwamba hakuna ushujaa Tanzania kwa mbunge kufungwa. Maana Tanzania ni nchi huru. Mbunge anapokuwa jela nchi inaathirika.

Gharama za kumpata mbunge kupitia uchaguzi ni kubwa sana. Mbunge anahudumiwa na nchi, analipwa mshahara na posho, matibabu, usafiri, dereva na kadhalika. Mbunge anapewa stahiki hizo ili afanye kazi za kujenga nchi. Badala afanye kazi iliyokusudiwa, anakuwa na hekaheka nyingi za polisi, mahakamani na kuhifadhiwa mahabusu.

Israel ni ushujaa kuwaweka jela wabunge wa Palestina. Maana kufanya hivyo wanakuwa wanadhoofisha dola ya Palestina. Wabunge wa Palestina ni ushujaa kushikiliwa mahabusu Israel, kwani ni harakati endelevu kuwakabili Waisrael.

Tanzania wabunge kuwa jela au kukamatwa mara kwa mara ni kujidhoofisha wenyewe kama taifa na kuwanyima wananchi uwakilishi bungeni.