Majaliwa awalilia watumishi watano Wizara ya Kilimo waliokufa ajalini

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema vifo vya watumishi hao vilivyotokana na ajali ya gari iliyotokea Manyoni wakati wakiwa kwenye majukumu yao vimemuumiza 

Singida/Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema vifo vya watumishi watano wa Wizara ya Kilimo waliofariki dunia papohapo katika ajali ya gari iliyotokea jana huko Manyoni vimemuumiza sana.

Watumishi hao walifariki dunia baada ya gari lao aina ya Mitsubishi Pajero kugongana uso kwa uso na lori.

Akihitimisha ziara yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Majaliwa alisema watumishi hao wamekufa wakati wakienda Mwanza kikazi.

Baadaye taarifa iliyotolewa na idara ya habari ya wizara hiyo ikisema,

Taarifa hiyo imewataja watumishi hao kuwa ni Stella Joram Ossano (39), Esta Tadayo Mutatembwa (36), Abdallah Selemani Mushumbusi (53), Charles Josephat Somi na Erasto Mhina (43).

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Sweetbert Njewike alisema ilitokea saa tano asubuhi katika Kijiji cha Njirii, Manyoni baada ya dereva wa gari la Wizara ya Kilimo kujaribu kuyapita malori mawili yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.

Alisema akiwa kwenye harakati za kuyapita malori hayo, ghafla alikutana uso kwa uso na lori lililokuwa likiendeshwa na Rubwata Kamanzi na kugongana.

Alisema lori hilo, mali ya kampuni ya Mount Meru lilikuwa likitokea Rwanda kuelekea Dar es Salaam.

Alitoa wito kwa maderava kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazogharimu vifo vya watu.

“Tumekuwa tukiimba mara kwa mara madereva kuendesha kwa mujibu wa mafunzo waliyopata. Wazingatie na kuzitii bila shurti sheria za usalama barabarani, lakini baadhi hawafanyi hivyo.”