Tigo ‘yatolewa’ sokoni

Makao Makuu ya Tigo jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Kampuni hiyo kongwe nchini, ambayo umiliki wake unahusishwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, pamoja na nyingine zinazotoa huduma za simu zinatakiwa zijisajili DSE kwa ajili ya kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesimamisha mchakato wa kuingiza hisa za Tigo katika soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya kuibuka mzozo wa umiliki wa kampuni hiyo ya huduma za simu nchini.

Kampuni hiyo kongwe nchini, ambayo umiliki wake unahusishwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, pamoja na nyingine zinazotoa huduma za simu zinatakiwa zijisajili DSE kwa ajili ya kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kwa mujibu wa sheria.

Lakini, wanasheria wa kampuni ya uwakili ya Brick Law House ya Uingereza wameiandikia CMSE wakidai kuwa mteja wao, ambaye ni Golden Globe International Services iliyosajiliwa visiwa vya British Virgin, ndiye anamiliki asilimia 99 ya hisa za Tigo na hajahusishwa katika mchakato huo wa kusajili hisa na hivyo kuufanya uwe batili.

Golden Globe na Millicon Tanzania NV ya Afrika Kusini zinagombea umiliki wa kampuni ya MIC inayoendesha huduma hiyo ya simu ya Tigo. Msemaji wa CMSA, Charles Shirima aliiambia The Citizen, ambayo ni gazeti dada la Mwananchi, kuwa kutokana na suala hilo kuwa mahakamani, mchakato wa kutathmini ombi la Tigo la kuorodheshwa DSE, umesitishwa.