‘Umbali ndiyo sababu ya wanafunzi kufeli Kigamboni’

Muktasari:

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kimbiji, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ambaye shule mbili kati ya sita zilizopata matokeo mabaya zinatoka jimboni kwake, alisema mkakati wa kujenga mabweni kila sekondari utasaidia kuondoa tatizo hilo.

Dar es Salaam. Wakati wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiendelea kujiuliza kwanini shule sita za mwisho katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana zimetoka katika jiji hilo, imeelezwa kuwa umbali kwenda shuleni ni moja ya sababu za matokeo hayo kuwa mabaya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kimbiji, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ambaye shule mbili kati ya sita zilizopata matokeo mabaya zinatoka jimboni kwake, alisema mkakati wa kujenga mabweni kila sekondari utasaidia kuondoa tatizo hilo.

Bweni hilo limejengwa na Kampuni ya Lake Cement kwa gharama ya Sh65 milioni ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushiriki wa maendeleo ya jamii (CSR).

Akizungumza kwenye makabidhiano hayo, Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo, Afroz Ansari alisema mbali na bweni, tayari wamejenga madarasa mengine mawili.