Likizo yakwamisha ushahidi kesi ya meno ya tembo

Muktasari:

Shauri hilo lilipangwa jana ili kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, lakini ilielezwa kuwa yupo likizo, hivyo  iliahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa. Sasa imepangwa kuanza kusikilizwa Januari 16, iwapo hakimu Saidi atakuwa amemaliza likizo.

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayohusu biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh5.4 bilioni inayomkabili raia wa China, Yang Feng Glan (66) na wenzake wawili imeshindikana kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka kutokana na hakimu kuwa likizo.

Shauri hilo lilipangwa jana ili kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, lakini ilielezwa kuwa yupo likizo, hivyo  iliahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa. Sasa imepangwa kuanza kusikilizwa Januari 16, iwapo hakimu Saidi atakuwa amemaliza likizo.

Yang maarufu malkia wa meno ya tembo na washtakiwa wengine Salvius Matembo (39) na Manase Philemon (39), wapo rumande tangu kesi hiyo ifunguliwe mahakamani hapo.

Ushahidi wa upande wa mashtaka ulipangwa kuanza Novemba 5, mwaka jana lakini ulikwama kutokana na shahidi aliyepangwa kuuguliwa na mkewe. Tangu wakati huo imekuwa ikiahirishwa hadi sasa.