Kigogo TRA atoa darasa Morogoro

Muktasari:

Kuchele amesema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara na kuwataka walipe walipe kodi bila kushurutishwa.

Morogoro. Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kuchele amesema ulipaji kodi kwa hiari unaweza kuifanya Serikali ikaondokana na utegemezi wa mataifa ya nje.

Kuchele amesema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara na kuwataka walipe walipe kodi bila kushurutishwa.

Amesema endapo kila mfanyabiashara atalipa kodi kwa hiari, lengo la kufikia uchumi wa kati kwa Tanzania litawezekana.

Kuchele amesema kama TRA inalo jukumu la kuhakikisha inaboresha na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabishara ikiwamo kuondoa malalamiko yanayotoka kwa watumishi wake kutumia lugha isiyo rafiki pindi wanapokusanya kodi.

“Morogoro ina mchango mkubwa kwenye pato la Taifa, imekuwa ikifanya vizuri na hii inatufanya TRA tuendelee kuuamini na kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa nguvu zote,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Muadhini Muyanza amesema ikiwa kuna malalamiko mengi yamekuwa yakitoka kwa watumiaji wa mashine za kielektroniki hasa mtu anapopata risiti na kufutika baada ya muda mchache jambo linalosababisha utunzaji wa kumbukumbu kuwa mdogo.