UCHAGUZI KENYA: Odinga kuwashughulikia mafisadi kama Magufuli

Mgombea urais kwa mwavuli wa Nasa, Raila Odinga akiwasili kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki juzi usiku kwa ajili ya mdahalo wa wagombea urais ambao ulisusiwa na mpinzani wake mkuu Rais Uhuru Kenyatta. Picha na Daily Nation.

Muktasari:

Awaambia mamilioni ya Wakenya waliokuwa wanafuatilia mdahalo wa wagombea urais kwamba endapo atashinda atatumia staili ya Rais Magufuli wa Tanzania kushughulikia walarushwa

 Nairobi, Kenya. Mgombea wa muungano wa upinzani (Nasa), Raila Odinga ameendelea kuonyesha anavyokunwa na utendaji wa Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya ufisadi akisema naye akiwa rais wa Kenya atashughulikia tatizo hilo kama Rais wa Tanzania.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alikuwa mshiriki pekee katika mdahalo wa juzi uliopangwa kwa wagombea urais baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoshiriki. Kutokana na hali hiyo, Odinga alitumia fursa hiyo kufafanua ahadi zake za kampeni kama vile kupunguza kodi na akasisitiza madai yake kwamba vyombo vya usalama vinashirikiana na utawala wa Jubilee kuiba Uchaguzi Mkuu.

Aliloulizwa na waongozaji mdahalo ni namna gani atapambana na rushwa akiwa madarakani, Odinga alisema ataiga staili ya Rais Magufuli anayetajwa kuwa swahiba wake.

Katika mdahalo huo, Odinga hakueleza kwa kina ni namna gani au alivutiwa vipi na Rais Magufuli.

Hata hivyo, Juni 27 mwaka huu alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni Kaunti ya Siaya, Odinga alifichua kwamba ataiga staili ya uongozi wa Rais Magufuli kwa kutokuwa na uvumilivu na walarushwa.

Tangu alipochaguliwa kuwa rais, mkuu huyo wa Tanzania akitumia staili aliyoibatiza “kutumbua majipu” alianza kupambana na wazembe kazini, maofisa wanaojihusisha na rushwa kwa kuwafukuza maofisa wa ngazi za juu ambao walikuwa wakijihusisha na ufisadi. Wengine walioshughulikiwa na Rais Magufuli ni walioshindwa kwenda na kasi yake na wapikaji ripoti.

Odinga aliapa kwamba atakaposhika madaraka ya nchi, atavunja mitandao ya ufisadi ambayo amedai inamzunguka Rais Kenyatta na Makamu wake William Ruto, na akaionya Jubilee ijiandae kwa mapambano kama ya sokwe mtu na mbwa.

Kituo cha kuhesabu kura

 Odinga alijitahidi kukwepakwepa kujibu maswali aliyoulizwa kuhusu ripoti kwamba wamefungua kituo cha kuhesabu kura nchini Tanzania.

Alipoulizwa kama mpango ulioripotiwa wa kuanzisha kituo cha kujumlishia kura Tanzania ambacho msemaji wa serikali ya Rais John Magufuli, Hassan Abbas amekanusha, kwanza alisita kisha akapuuza.

“Baadhi ya vitu ni vya kufikirika akilini mwa watu. Kwa nini tuwe na kituo cha kujumlishia kura Tanzania?” alihoji.

Alisema uamuzi wa mahakama kwamba matokeo yaliyojumlishwa jimboni ni ya mwisho na vyama vikajumlisha matokeo yao, hakutakuwa na sababu ya kuhofia.

“Kwa nini mtu ahofie kituo cha kujumlishia kura kiwe Ujerumani, Tanzania au hata mwezini? Wala hiyo isiwe hoja,” aliongeza.

Alipobanwa ajibu swali hilo bayana, alisema: “Tuna kituo cha kujumlishia kura Kenya na mawinguni.”

Mapambano na Al Shabaab

Pia, Odinga alimsakama Rais Kenyatta hasa kwa tukio ambalo Al Shabaab ilifanya shambulizi wakati mkuu wa nchi alikuwa nje ya nchi.

“Ikiwa nitakuwa rais sitakuwa nikiangalia shindano la Formula 1 Dubai wakati watu wanashambuliwa na Al Shabaab. Nitakuwa mstari wa mbele nikiongoza mapambano,” alisema Odinga.

Odinga aliongeza: “Wakati wa sikukuu za kitaifa tunaonyeshwa silaha nyingi sana. Lakini hazionekani wakati yakifanyika mashambulizi ya kigaidi.”

Afichua siri ya kushiriki

Mapema Odinga alisema alikubali kushiriki mdahalo baada ya kuhakikishiwa kuwa hatasimama jukwaa moja na wagombea wasio na matumaini ya kushinda.

Aliwaambia waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki kwamba alijisikia kama mchezaji wa mpira wa miguu aliyefunga bao la goli lisilo na kipa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukwepa tukio hilo.