Ummy Mwalimu awajia juu Ma-RC, DC

Muktasari:

 

  • Wakuu wa mikoa na wilaya kuacha tabia ya kuwaweka mahabusu watumishi wa umma kwa makosa ya kitaaluma.
  • Makosa yanapaswa kushughulikiwa na mamlaka wanazofanya kazi.
  • Utumishi wake kama waziri amekusudia kuacha kumbukumbu katika kuimarisha afya ya uzazi na mtoto.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kuacha tabia ya kuwaweka mahabusu watumishi wa umma kwa makosa ya kitaaluma.

Ummy ametoa wito huo leo Jumatatu mjini Bagamoyo wakati akizindua majengo ya wodi ya wazazi na matibabu ya dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ambayo yamejengwa kwa udhamini wa Taasisi ya Kiisilam ya Dhi Nureyn.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majidi Mwanga na Mbunge wa Bagamoyo, Dk Shukuru Kawabwa, madiwani na viongozi wa CCM wa wilaya hiyo.

Ummy amesema makosa kama hayo yanapaswa kushughulikiwa na mamlaka wanazofanya kazi lakini kitendo cha kuwaweka ndani kinawaondolea morali na ari ya kufanya kazi.

"Nakushukuru Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo sijawahi kusikia umefanya kitendo cha namna hiyo. Ukiona makosa ya kitaaluma wewe walete juu tutawashughulikia," amesema Ummy.

Amesema katika utumishi wake kama waziri amekusudia kuacha kumbukumbu katika kuimarisha afya ya uzazi na mtoto.

"Ndiyo maana katika ziara zangu huwezi kuniona nimeingia kwenye 'general ward' au wodi ya wanaume badala yake napita katika wodi ya wazazi, watoto na famasi sio kwamba wanaume nawadharau hapana, mambo ni mengi na huwezi kuyashika yote kwa pamoja mimi nimeamua kujikita katika kuimarisha afya ya uzazi na watoto," amesema.