Utafiti: Asilimia 60 ya wananchi hawapo huru kumkosoa Rais

Muktasari:

Takwimu za muhtasari huu zinatokana na utafiti wa Sauti za Wananchi ambao huratibiwa na taasisi ya Twaweza.

Dar es Salaam. Utafiti mpya uliotolewa leo na Taasisi ya Twaweza, umebaini kuwa asilimia 60 ya wananchi, hawajisikii huru kukosoa Taasisi ya Rais, huku asilimia 54 hawajisikii huru kumkosoa Makamu wa Rais.

Taarifa iliyotumwa na taasisi hiyo kwa vyombo vya habari leo Machi 29, imeeleza kuwa idadi kubwa ya wananchi wamesema wanapaswa kuwa huru kuikosoa Serikali na Taasisi ya Rais inapofanya uamuzi mbaya.

Matokeo hayo yametolewa na Twaweza katika muhtasari wake uitwao; ‘Siyo kwa kiasi hicho’? Maoni ya wananchi kuhusu taarifa na mijadala.

Takwimu za muhtasari huu zinatokana na utafiti wa Sauti za Wananchi ambao huratibiwa na taasisi ya Twaweza.

Katika matokeo hayo, idadi kubwa ya wananchi (87%) wamesema wanapaswa kuwa huru kuikosoa Serikali na Taasisi ya Rais inapofanya uamuzi mbaya na kutosikiliza ushauri (80%).

Wanaamini kupitia ukosoaji wanaweza kuisaidia Serikali kutofanya makosa (81%) na si kuwashushia hadhi watendaji wa umma, au kuhatarisha umoja (19%).

Vilevile wananchi hawaungi mkono matumizi ya lugha ya matusi, asilimia 71 ya Watanzania hawataki wananchi waruhusiwe kuwaita wafuasi wa chama chochote cha siasa “wapumbavu au malofa”.

Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Una uwakilishi wa Tanzania Bara pekee, Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu. Kwa maelezo zaidi kuhusu mbinu za utafiti huu tembelea www.twaweza.org/sauti.

Takwimu za muhtasari huu zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,519 kutoka awamu ya 25 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, na zilikusanywa kati ya Novemba 7 na Novemba 27 mwaka 2017.

Kadhalika, utafiti huo ulibaini kuwa wananchi wengi wana imani kubwa na taarifa zinazotolewa na Rais (70%) na Waziri Mkuu (64%). Idadi ndogo zaidi wanamwamini mwenyekiti wao wa kijiji (30%), wabunge (wa chama tawala 26%, wa upinzani 12%), na viongozi wa Serikali kwa ujumla (22%).