VIDEO: Waziri, RC na Kamati ya ulinzi na usalama wapangua mawe saa nzima

Muktasari:

Tukio hilo limetokea leo Julai 16 saa 2:00 wakati Kigwangala, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Mara  na viongozi wengine wa Serikali na kisiasa wilaya ya Tarime walipokuwa wakitoka ndani ya hifadhi baada ya kukagua mipaka katika eneo lenye mgogoro kati ya hifadhi na vijiji jirani.

Tarime. Msafara wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala umekwama kwa muda wa saa nzima eneo la Kegona ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) baada ya watu wasiojulikana kupanga rundo la mawe makubwa katikati ya barabara.

Tukio hilo limetokea leo Julai 16 saa 2:00 wakati Kigwangala, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Mara  na viongozi wengine wa Serikali na kisiasa wilaya ya Tarime walipokuwa wakitoka ndani ya hifadhi baada ya kukagua mipaka katika eneo lenye mgogoro kati ya hifadhi na vijiji jirani.

Viongozi walilazimika kuteremka kwenye magari na kuanza kazi ya kuyaweka pembeni mawe hayo, kazi iliyochukua saa 3:15 usiku.

Akizungumzia tukio hilo, Kigwangala amelaani waliopanga mawe hayo barabarani akiwaita wenye nia ovu dhidi ya Juhudi za Serikali za kutatua mgogoro huo.

'Hawa (waliopanga mawe barabarani) walitaka msafara wangu ulale porini; nimekuja kwa mapenzi mema kuona namna gani tutatatua mgogoro huu badala yake nazuiliwa kupita kwa kupangiwa mawe," amesema na kuhoji' Kigwangala

Waziri na msafara wake wameendelea na safari kuelekea wilayani Serengeti.