Akamatwa akiwa amevalia sare za polisi

Kijana Abubakar Mbaya (21) mkazi wa Mkoa wa Morogoro akiwa katika kituo cha Polisi mjini Kibaha baada ya kukamatwa kwa kosa la kukutwa amevaa sare za Jeshi la Wananchi JWTZ huko kwa Mathias huku yeye sio askari ndani ya basi la abiria mali ya kampuni ya Abood ambapo alikua anasafiri kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar esalaam, katika mahojiano kijana huyu amedai sare hizo za marehemu babu yake na yeye amezivaa kwa upendo tu kwani toka anakua alitamani sana kuwa askari wa JWZT
Picha na Julieth Ngarabali

Muktasari:

  • Vijana wameendelea kukamatwa mjini Kibaha wakiwa wamevaa sare  za majeshi kinyume cha sheria.

Kibaha. Josephat Hongati (23) mkazi wa Ngokoro A mkoani Shinyanga amekamatwa mjini Kibaha mkoani Pwani akiwa amevalia sare za Jeshi la Polisi akijinasibu yeye ni askari wa jeshi hilo.

Kijana huyo amejinasibu mbele ya baadhi ya ndugu zake wa karibu kuwa yeye ni askari wa depo ya H 3 ambaye anafanyakazi wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Askari feki huyo alikamatwa jana jioni Septemba 20, 2018 katika mtaa wa Loliondo kilipo kituo kipya cha muda cha daladala mjini Kibaha.

Kamanda wa Polisi Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kijana huyo akiwa amevalia sare hizo kinyume cha sheria alikamatwa baada ya kutiliwa shaka na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa Loliondo.

Alisema baada ya kukamatwa alifikishwa kituoni na kuhojiwa zaidi ambapo amekiri kuwa yeye si askari wa jeshi hilo.

Nyigesa alibainisha katika uchunguzi wa awali, wamebaini kijana huyo amekuwa akijifanya askari katika mikoa mbalimbali nchini kwa vipindi tofauti.

Katika uchunguzi huo, polisi wamebaini kijana huyo amewahi kukamatwa mkoani Shinyanga Julai 30, 2018 kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Kamanda huyo alisema kijana huyo alifikishwa mahakamani Shinyanga kwa kosa hilo ambapo alipata dhamana na mpaka sasa kesi yake bado inaendelea.

Alisema kijana huyo baada ya kuulizwa alipozipata sare hizo alidai ameiba za rafiki yake ambaye ni askari na alikwenda kumtembelea kwake na amekuwa akizivaa kujifanya askari katika kuwababaisha watu mitaani anapoona wamefanya makosa.

“Huyu kijana ni bingwa wa utapeli huu wa kutumia sare za majeshi. Maana taarifa tulizopata kwanza amekua anajinasibu hata kwa jamaa zake wa karibu yeye ni polisi wa Depo ya H3 na anafanya kazi Kasulu,” alisema Nyigesa.

Kamanda huyo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika upelelezi wakati wowote kuanzia sasa ili kujibu mashitaka dhidi yake.

Hili ni tukio la pili kutokea mjini Kibaha ndani ya saa 48, juzi kijana mmoja mkazi wa Morogoro Abubakari Mbaya (22) alikamatwa akiwa amevalia sare za JWTZ.

Mbaya alipohojiwa alisema ni za marehemu babu yake na amevaa kwa upendo alionao kwa jeshi hilo toka utotoni.