Amuua mke wake kwa mundu, naye auawa

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Sweetbert  Njewike.

Muktasari:

Wanandoa hao walikuwa wakizozana na kushutumiana kutoka nje ya ndoa.

Singida. Mkazi  wa kijiji cha Kinku  tarafa ya Mungaa wilaya Ikungi , Singida, Editha Kanisi (49) ameuawa kwa  kukatwa kwa  kisu cha kukatia majani, (mundu) shingoni na kichwani na mume wake Joseph Wilbroad (53).

Baada ya Joseph kufanya mauaji hayo wananchi wenye hasira kali nao walimshambulia kwa silaha na kumuua.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo  Agosti 16 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Sweetbert  Njewike amesema tukio hilo limefanyika jana Agosti 15 mwaka huu usiku saa mbili huko katika kijiji cha Kinku.

Amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana usiku wakati  wanandoa hao wakijiandaa kulala na uliibuka mzozo mkali baina yao huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa si mwaminifu kwenye ndoa.

“Kila mmoja alimtuhumu mwenzake kutokuwa mwaminifu katika ndoa yao,”amesema.

Akifafanua zaidi amesema malumbano hayo yalisababisha mwanaume kuchukua kisu cha kukatia majani kiitwacho mundu na kumkata mke wake shingoni na kichwani.

Amesema Editha alijaribu kukimbia lakini alipotoka nje ya nyumba yao alianguka chini na kufariki dunia papo hapo.

 “Watoto wao baada ya kuona mama yao kaanguka chini, walianza kupiga kelele za kuomba msaada na majirani walifika mara moja kwenye eneo la tukio na wakamwomba Joseph afungue mlango,” amesema Kamanda huyo

"Joseph alikaidi kufungua mlango na ndipo walipouvunja kwa nguvu.Walipofanikiwa kumkamata Joseph,walimpiga kwa silahaza jadi na kusababisha kifo chake,”ameongeza.

Amesema uchunguzi zaidi na msako mkali unaendelea kuwasaka waliohusika na mauaji ya Joseph.