Prime
Makada CUF wapanga kuandamana, Msajili atoa kauli
Muktasari:
- Makada wanaotaka kuandamana na wafuasi wao ni wale waliowasilisha barua za malalamiko yao katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa nyakati tofauti wakitaka uchaguzi mkuu uliofanyika Februari 22 mwaka huu uliomchagua Yusuf Mirambo na viongozi wengine ubatilishwe, wakidai uligubikwa na kasoro mbalimbali za kimchakato.
Dar es Salaam. Wakati makada wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) wakijiandaa kuandamana pamoja na wafuasi wao kutinga Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kudai mrejesho wa malalamiko yao ya kutaka kubatilishwa kwa uchaguzi mkuu uliouweka madarakani uongozi mpya wa chama hicho, Ofisi ya Msajili imewataka makada hao kuwa watulivu na kuepuka kuweka shinikizo.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Juni 23, 2026, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema majibu ya malalamiko yao bado yanafanyiwa tathmini, hivyo makada hao wanapaswa kusubiri mchakato huo ukamilike kabla ya kupatiwa majibu rasmi.
“Niwasihi makada hao wawe watulivu. Ofisi ya Msajili bado inapitia majibu yaliyowasilishwa na uongozi wa chama chao. Baada ya kujiridhisha na maelezo hayo, tutatoa majibu na msimamo wetu. Kwa sasa wapunguze presha,” amesema Nyahoza.
Wakati huohuo, uongozi wa CUF umesema hoja zote zilizowasilishwa na makada hao tayari zilijibiwa na majibu yake kuwasilishwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa muda mrefu uliopita.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa CUF, Yusuf Mirambo, amesema barua mbili za malalamiko zilizowasilishwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo zilijibiwa kwa wakati, na majibu yake kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Malalamiko hayo yaliwasilishwa kwa nyakati tofauti na makada wa chama hicho, Othman Omar Dunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Bara, pamoja na Romanus Mapunda. Wawili hao wanataka uchaguzi mkuu uliomchagua Mirambo na viongozi wengine ubatilishwe wakidai uligubikwa na kasoro mbalimbali za kimchakato.
Dunga, ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Mirambo katika uchaguzi huo, alidai baadhi ya wajumbe walioshiriki kupiga kura hawakuwa na sifa za kisheria za kushiriki uchaguzi huo.
Kwa upande wake, Mapunda alidai alinyimwa fursa ya kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti, jambo ambalo alisema lilimzuia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi uliofanyika ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Uchaguzi huo ulifanyika Februari 22, 2026 baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uchaguzi wa mwaka 2024 uliokuwa umemweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.
Mirambo amesema chama kilipokea barua za malalamiko kutoka kwa makada hao wawili kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wakipinga uchaguzi mkuu uliomweka yeye na viongozi wenzake madarakani.
Amesema ingawa kila barua ilikuwa na hoja zake mahsusi, lengo kuu la walalamikaji lilikuwa moja; kutaka uchaguzi mkuu wa Februari 22 mwaka huu ufutwe na kuitishwa uchaguzi mwingine.
“Tulijibu barua zote ndani ya muda tuliopangiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, na majibu yetu yako kwa Msajili. Ninachoweza kusema ni kwamba chama kilijibu hoja zote, na kama mwenyekiti niliyapitia na kuyaidhinisha,” amesema Mirambo.
Amesema majibu hayo yaliwasilishwa Mei 14 mwaka huu kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ingawa hana taarifa kama walalamikaji walishafikishiwa majibu hayo.
Naye Othman amesema wanakusudia kuandamana kwenda Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wiki hii ili kushinikiza kupatiwa majibu ya malalamiko yao, akidai kuwa imepita muda mrefu tangu wayawasilishe bila kupata mrejesho.
“Alhamisi ya wiki hii tutaenda Ofisi ya Msajili Dar es Salaam tukiwa na wafuasi wetu kushinikiza kupewa majibu yetu. Tunaamini madai yetu ya kutaka uchaguzi mkuu uliopita ubatilishwe yana msingi, na tunashangazwa na kuchelewa kwa majibu,” amesema Othman.
Kwa mujibu wake, kuendelea kwa uongozi anaouona kuwa haukuchaguliwa kihalali ni ishara ya kudhoofika kwa misingi ya demokrasia ndani ya chama hicho, huku akisisitiza kuwa wanachotaka ni viongozi waliochaguliwa na wanachama halali.
“Katika barua yangu niliwasilisha ushahidi wa kutosha unaounga mkono malalamiko yangu. Ninaamini Mirambo hakuchaguliwa na wajumbe halali wa chama, na tunashangazwa na ukimya wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu suala hili,” amesema Othman.