VIDEO-Anna asema huenda habari za mauaji ndizo zilizimpoteza mumewe

Muktasari:

  • Anna amesema  pamoja na kuhisi hivyo lakini bado hawaelewi kwa kuwa wamekuwa wakihisi mara hiki mara kile.

Kibiti. Mke wa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Mwananchi wilayani Kibiti, Anna Pinoni amesema kuwa anahisi kupotea kwa mume wake Azory Gwanda inaweza kuwa ni kutokana na habari za mauaji alizokuwa anaandika wilayani humo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Anna amesema  pamoja na kuhisi hivyo lakini bado hawaelewi kwa kuwa wamekuwa wakihisi mara hiki mara kile.

Hata hivyo, amesema kwa kuwa hawaelewi wanamsubiri Azory mwenyewe akirudi ndiye atakayewaeleza alichukuliwa kwa ajili ya nini.

Wakati Anna akisubiri, Baraza la Habari Tanzania (MCT), limesema limestushwa na taarifa za kupotea kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi wa mkoa wa Pwani, Azory Gwanda.

Akizungumza na gazeti hili leo Jumanne, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema wamestushwa na hali hiyo na kusema kuwa kazi ya uandishi siyo salama sana kwa hali ya sasa.

“Huu ni ushahidi mwingine kazi ya uandishi wa habari ni ya hatari na mashaka. Siyo Azory kuna mwandishi mwingine wa  Kasulu (Kigoma) na yeye alipotea na matukio mengine ya kutishwa na kuwekwa ndani kwa wanataaluma hii,” amesema Mukajanga.

Mukajanga amesema ni wakati muafaka kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, kulinda usalama wa waandishi wao na mwaka kesho MCT itaweka program ya mafunzo kwa wanahabari kwenye mazingira hatarishi.

Hata hivyo, Mukajanga alivitaka vyombo vya dola kuendelea kumtafuta mwandishi  huyo.