Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaweka mfumo rahisi kwa wazalishaji

Ofisa Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Kazi, Odo Hekela akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miongozo ya ya ukuaji wa uchumi endelevu kwa wazalishaji wadogo Jijini Dodoma leo Julai 20, 2026. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Serikali imeanza maandalizi ya Mwongozo wa Ukuaji wa Uchumi Endelevu utakaowasaidia wazalishaji na wasindikaji wadogo kujitathmini na kutimiza viwango vya mazingira, kazi, afya na ubora wa bidhaa kabla ya ukaguzi rasmi, hatua inayotarajiwa kupunguza urasimu na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.

Dodoma. Serikali imeanza kuandaa mwongozo wa ukuaji wa uchumi endelevu unaolenga kuwasaidia wazalishaji na wasindikaji wadogo, kutekeleza viwango vinavyohitajika bila kukabiliwa na changamoto ya kukaguliwa na taasisi nyingi za serikali kwa wakati mmoja.

Mwongozo huo unalenga kuunganisha mifumo ya usimamizi wa mazingira, kazi, hifadhi ya jamii, kilimo na misitu ili kuweka utaratibu mmoja utakaorahisisha utekelezaji wa matakwa ya kisheria kwa wazalishaji, wawekezaji na wafanyabiashara wadogo.

Akizungumza leo Jumatatu, Julai 20, 2026 jijini Dodoma katika kikao cha wadau kilichojadili mwongozo huo, Ofisa Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Kazi, Odo Hekela amesema hatua hiyo inalenga kupunguza malalamiko ya wazalishaji wanaodai kukabiliwa na masharti mengi kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

Amesema lengo la Serikali si kuwa kikwazo kwa wazalishaji, bali kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

“Nia yetu ni kumwezesha mzalishaji kujitathmini mwenyewe kabla Serikali haijafika kufanya ukaguzi. Serikali haiwekwi kuwa kikwazo, bali inalinda ubora wa bidhaa na uzingatiaji wa viwango,” amesema Hekela.

Amefafanua kuwa katika soko la kimataifa, bidhaa zinahitaji kuwa na uthibitisho kuwa zimetengenezwa kwa kuzingatia masuala ya mazingira, haki za wafanyakazi, afya na usalama kazini pamoja na viwango vya ubora.

Kwa mujibu wa Hekela, changamoto kubwa kwa wazalishaji wadogo si kukataa kufuata sheria, bali ni kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu mahitaji yanayohusu mazingira, ajira, mikataba ya kazi, mishahara, usalama mahali pa kazi na kuzuia ajira kwa watoto.

“Tunahitaji mzalishaji ajione kama anavyojiangalia kwenye kioo. Ajue mapema kama ametimiza viwango vinavyotakiwa kabla ya kufanyiwa ukaguzi. Hilo litapunguza urasimu na kuongeza ushindani wa bidhaa zetu katika masoko ya kimataifa,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mkoa wa Morogoro, Joyce Omolo amesema mwongozo huo umekuwa nyenzo muhimu katika kurahisisha utekelezaji wa sheria za mazingira kwa kuwawezesha wawekezaji na wazalishaji kufahamu na kutekeleza matakwa ya kisheria mapema.

Amesema mfumo huo umesaidia kupunguza muda wa ukaguzi kwa sababu wawekezaji wengi hujihakiki na kurekebisha maeneo yenye mapungufu kabla ya maafisa kufika katika maeneo yao ya uzalishaji.

“Kazi ambayo zamani ingeweza kuchukua siku tatu au nne sasa inaweza kukamilika ndani ya siku mbili kwa sababu mwekezaji tayari ameshazingatia matakwa ya sheria. Sisi tunafanya uhakiki tu,” amesema Omolo.

Amesema utaratibu huo unaongeza ufanisi kwa kuwa unahamisha sehemu ya jukumu la uzingatiaji wa sheria kwa wazalishaji wenyewe, huku serikali ikiendelea kuwa na nafasi ya kusimamia na kuthibitisha utekelezaji.

Naye Ofisa Mradi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Samuel Kajiba, amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kutekeleza dhana ya ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu utasaidia kuongeza uzalishaji huku ukilinda mazingira.

Amesema hatua hiyo pia itasaidia kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia matumizi bora ya rasilimali na mifumo endelevu ya uzalishaji.

Kajiba amesema IUCN inaendelea kutekeleza mradi wa SUSTAIN unaolenga kujenga mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula, kuhifadhi afya ya mandhari na kulinda mifumo ya ikolojia.

Amesema mradi huo ulianza mwaka 2024 na awamu ya kwanza inatarajiwa kuendelea hadi mwaka 2030, huku awamu ya pili ikipangwa kuendelea hadi mwaka 2036.

“Dhana hizi zinatusaidia kuhakikisha tunakuwa na mazingira stahimilivu, kulinda afya ya ardhi, vyanzo vya maji na mifumo ya ikolojia, pamoja na kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Ameongeza kuwa lengo kubwa ni kuifanya dhana hiyo kuwa sehemu ya utekelezaji wa kitaifa ili Tanzania iwe na mfumo unaounganisha ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo itaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakwenda sambamba na ulinzi wa mazingira na ustawi wa jamii.