Azma ya kuhama Dar ilikuwapo tangu enzi za mkoloni Mjerumani

Muktasari:

Katika kujibu maswali hayo, Profesa Lussuga Kironde anaeleza katika kitabu chake kinachoitwa “Will Dodoma Ever Be the New Capital of Tanzania?” Kwamba suala la kuhamisha makao makuu ya Tanzania lilikuwapo tangu wakati utawala wa mkoloni Mjerumani (1884 - 1917).

Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikichachamaa kuhamia Dodoma, watu wamekuwa wakijiuliza kwamba wazo la kuhamia Dodoma lilitoka wapi? Sababu zipi ziliufanya mji huo kuchaguliwa kuwa makao makuu ya Tanzania? Kwa nini mpango huo haukutekelezwa kwa muda mrefu?

Katika kujibu maswali hayo, Profesa Lussuga Kironde anaeleza katika kitabu chake kinachoitwa “Will Dodoma Ever Be the New Capital of Tanzania?” Kwamba suala la kuhamisha makao makuu ya Tanzania lilikuwapo tangu wakati utawala wa mkoloni Mjerumani (1884 - 1917).

Mwaka 1891, serikali ya Mjerumani ilichagua mji wa Dar es Salaam kuwa makazi yao badala ya mji wa Bagamoyo ambao ulikuwa na bandari nzuri. Sababu kubwa ilikuwa kwamba mji wa Dar es Salaam ulikuwa na mazingira mazuri kwa wao kuishi.

Wakati wa vita ya Kwanza ya Dunia, Serikali ya Mjerumani ililazimika kuondoka Dar es Salaam kwenda Tabora, wakati huo wazo la kuhamisha moja kwa moja makao makuu ya Serikali liliwajia.

Mwaka 1916, Gavana wa wakati huo, Dk Heinrich Schenee alifanya tafiti katika maeneo ya Buda na Kisi, kandokando ya bonde la mto Romuma (Mpanda Mashariki). Katika utafiti huo alibaini kwamba maeneo hayo yanafaa kuwa makao makuu kwa sababu hayakuwa na mbu wala mbung’o.

Wakoloni walizingatia zaidi maeneo ambayo ni mazuri kwao kuishi na ambayo yangewafanya waishi bila kuugua magonjwa. Wakoloni waliyapenda maeneo ya Tabora, hivyo walipendelea ndiyo kuwapo mji mkuu.

Dk Schnee aliagiza uchunguzi zaidi wa eneo hilo hasa ardhi yake kwa ujenzi na upatikanaji wa maji kwa ajili ya kuhamisha serikali moja kwa moja. Hata hivyo mpango huo haukutekelezwa mpaka Mjerumani alipoondolewa nchini baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia.

Utawala wa Mwingereza

Suala la kuhama Dar es Salaam liliendelea pia katika utawala wa Mwingereza. Mwaka 1927, Gavana wa Uingereza nchini, Donald Cameron aliunda kamati maalumu kwa ajili ya kuchunguza eneo linalofaa kwa ajili ya makazi na makao makuu ya idara mbalimbali za serikali.

Utulivu unahitajika

Moja ya hadidu za rejea alizoipatia kamati hiyo ni kuangalia uwezekano wa kuhamisha makao makuu ya idara za serikali kutoka Dar es Salaam. Cameron aliiambia kamati hiyo kwamba:

“Ni vema kuweka akilini kwamba Dar es Salaam haitaendelea kuwa makao makuu ya serikali wakati wote. Haiwezi kuwa hivyo, lazima ipatikane sehemu nzuri kiafya na yenye utulivu huko bara.”(ameandika Profesa Kironda);

Wakuu wa idara walikuwa hawataki kuhama Dar es Salaam, hata hivyo idara ya mifugo ilihamia Mpwapwa, idara ya kilimo na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mashariki zilihamia Morogoro, mwishoni mwa miaka ya 1920.

Wakati huo mitazamo ya wakuu wa idara na wakuu wa mikoa ilikuwa tofauti na walipendekeza maeneo kadhaa ambayo yangefaa kuwa makao makuu ya serikali. Maeneo hayo ni Arusha, Dodoma, Iringa, Lushoto, Manyoni, Morogoro, Moshi, Mpwapwa, Mwanza na Tabora.

Kwanini Dodoma?

Kati ya miji hiyo Dodoma ndiyo eneo pekee lililoonekana kwamba linafaa kwa sababu linafikika kirahisi. Changamoto za mji wa Dodoma kama vile uhaba wa maji na hali ya jangwa vilibainika lakini havikuondoa sifa ya mji huo.

Siyo watu wote walikubaliana na mpango wa kuhama Dar es Salaam. Katibu wa Mambo ya Ndani (SNA) na Mkurugenzi wa Huduma za Afya (DMS) walipinga mpango huo kwa hoja kwamba itakuwa ni gharama kubwa na si jambo zuri kutenganisha mji wa kibiashara na makao makuu ya serikali.

Mwaka 1959, suala la kuhamisha makao makuu liliibuka tena bungeni baada ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (Legislative Council) kujadili suala hilo. Awali kila mjumbe alipendekeza mji wake kuwa makao makuu lakini baadaye walikubaliana kuwa Dodoma ndiyo inafaa kuwa makao makuu kwa sababu iko katikati ya nchi.

Mipango baada ya uhuru

Profesa Kironda anaendelea kusimulia katika kitabu chake kwamba mwaka 1966 Joseph Nyerere (ndugu wa Mwalimu Julius Nyerere) aliwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka serikali ihamie Dodoma.

Ili kupunguza gharama za kutekeleza mpango huo, alipendekeza kwamba serikali ihame kwa awamu. Hata hivyo, mjadala huo ulikwamishwa na suala la gharama. Makamu wa Rais Rashid Kawawa aliahirisha mjadala huo na kusema suala hilo linahitaji mjadala mpana utakaowashirikisha wananchi.

Mwaka 1972 Kamati Kuu ya Tanu mkoa wa Mwanza (MRCC) ilitoa mapendekezo kwa Kamati Kuu ya Taifa (NCC) kwamba makao makuu ya chama yawe Dodoma ili kukisogeza chama karibu na wananchi.

Walisema sababu hiyo ingeifanya pia serikali ihamie Dodoma kwa sababu chama na serikali vilikuwa ni kitu kimoja.

MRCC ilieleza kwamba Dodoma ni katikati ya nchi, ina hali nzuri ya hewa, ni sehemu nzuri kwa mawasiliano na sehemu salama dhidi ya mashambulizi kutoka nje. Pia, kamati hiyo ilieleza kwamba Dodoma itakuwa kitovu cha serikali katika jitihada zake za kukuza ujamaa kwa sababu iko karibu zaidi na wananchi.

Kamati Kuu (NCC) ilitoa mwongozo kwamba suala hilo lijadiliwe kitaifa ili kufikia uamuzi. Kura ya maoni ilipigwa katika matawi yote ya Tanu nchi nzima. Kati ya matawi 1859 yaliyopiga kura, matawi 1057 (asilimia 54) yaliridhia makao makuu kuwa Dodoma na matawi 842 (asilimia 46) yalipinga mpango huo.

Katika ngazi ya mkoa, mikoa 18 iliridhia mpango wa kuhamia Dodoma na mikoa mitatu (ukiwamo wa Dar es Salaam) ilipinga mpango huo. Kutokana na kura hizo, Kamati Kuu iliamua kuhamia Dodoma ndani ya miaka 10.

Oktoba Mosi 1973, Mwalimu Nyerere alihutubia Taifa kwa njia ya redio kutangaza uamuzi huo akisema suala la gharama ni la muda mfupi tu lakini makao makuu yatakuwa yakudumu. Alisema kuendelea kuchelewesha mpango huo, ndivyo gharama zinavyoongezeka.

Rais alitangaza kuanzisha vyombo viwili; kwanza ni Wizara ya Maendeleo ya Mji Mkuu kwa ajili ya kuratibu mpango wa serikali kuhamia Dodoma; na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.

Mpango wa kuhamia Dodoma ulikadiriwa kufanyika ndani ya miaka 10 kuanzia mwaka 1976 na kugharimu Sh3.71 bilioni (Dola za Marekani 53 milioni).

CDA ilitakiwa kupata Sh371 milioni kila mwaka kutoka serikalini, lakini serikali imekuwa haitoi fedha hizo.

Nchi zilizofanikiwa kuhama

Tanzania siyo nchi ya kwanza kuhamisha makao makuu ya serikali yake, zipo nchi nyingine zilizofanikiwa kufanya hivyo. Baadhi ya nchi hizo ni Malawi (kutoka Zomba kwenda Lilongwe), Nigeria (kutoka Lagos kwenda Abuja) na Ivory Coast, kutoka (Abidjan kwenda Yamousoukou).

Nchi zote hizo zilitengeneza sera maalumu za kuanzisha miji mikuu, lakini Tanzania haikuweza kuhamisha makao yake makuu kutokana na sababu za kisiasa na kiuchumi.

Profesa Kironde anasema kuwa tatizo lililopo ni viongozi kutokuwa na dhamira ya dhati kuhama Dar es Salaam, vipaumbele visivyo sahihi kwa CDA na maofisa wa serikali kutokuwa tayari kuhamia Dodoma.

Anasema mwamko wa viongozi na dhamira ya kweli ndiyo msingi wa utekelezaji wa azimio la serikali kuhamia Dodoma. Serikali haiwezi kuhama kama viongozi wake wa juu hawana utayari wa kuhama.