Miili ya askari tisa kuagwa viwanja vya JWTZ Migombani

Muktasari:

Askari hao ni kati ya 14 waliouawa Desemba 7,2017 nchini DRC.

Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ataongoza waombolezaji kuaga miili ya askari tisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliofariki dunia wakilinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Taarifa ya Naibu Mkurugenzi Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar, Juma Salum Mohamed imesema shughuli ya kuaga miili hiyo itafanyika katika viwanja vya JWTZ Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kuanzia saa nane mchana wa leo Alhamisi Desemba 14,2017.

Mohamed katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano Desemba 13,2017 alisema leo saa 6:30 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume (Terminal I) watawasili viongozi wa Serikali na ndugu wa marehemu walioshiriki kuaga miili ya askari hao Dar es Salaam.

Amesema miili ya askari hao itawasili uwanjani hapo saa 7:30 mchana na itapelekwa katika viwanja vya Jeshi Migombani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Balozi Idd atatoa salamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed akitoa salama za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi alisema wamepokea kwa masikitiko vifo vya askari hao.

Alisema Serikali na wawakilishi kwa jumla wanaungana na ndugu, jamaa, askari na Serikali ya Muungano katika msiba huo ambao unahusu jamii nzima ya Tanzania.

Miili ya askari 14 kati yao watano wa Tanzania Bara ilirejeshwa nchini kwa ndege ya Umoja wa Mataifa Desemba 11,2017.

Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa alisema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa takriban saa 13.

Alisema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 walijeruhiwa na wengine wawili  hawajulikani walipo. Taarifa iliyotolewa baadaye na jeshi ilisema askari mmoja amepatikana.

Mwakibolwa alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu nchini DRC.