Benki ya Dunia yashikilia Sh112 bilioni za msaada ikitaka kuboreshwa sheria ya takwimu

Muktasari:

Benki ya Dunia inazishikilia Sh112 bilioni zinazotarajiwa kuboresha mfumo wa ukusanyaji, uchakataji na utunzaji wa takwimu katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Benki hiyo haijaridhishwa na mabadiliko yaliyoyomo kwenye muswada unaokusudia kuiboresha Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.


Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imezuia msaada wa Dola 50 milioni za Marekani (zaidi ya Sh112 bilioni) kwa Tanzania ikitaka majadiliano zaidi kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa kwenye Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Fedha hizo zilikuwa msaada wa kuisaidia Serikali kuboresha mfumo wa kukusanya, kuchakata na kutunza kumbukumbu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) lakini benki hiyo inaamini kuna vifungu vinavyokandamiza uhuru wa kujieleza.

Taarifa iliyochapishwa Oktoba Mosi na mtandao wa Eye on Global Transparency’ inasema Benki ya Dunia inasikitishwa na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na mwenendo wa demokrasia.

Ofisa habari wa Benki ya Dunia nchini, Loy Nabeta alithibitisha taarifa hiyo: “Taarifa ya Benki ya Dunia ilikuwa inajibu maswali yaliyoulizwa na mtandao wa freedom.org.”

Muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Takwimu ulipitishwa Septemba 10  na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao, pamoja na mambo mengine, unakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu za Serikali.

Adhabu ya kufanya hivyo ni  faini ya Dola 6,000 au kwenda jela miaka mitatu. Vilevile, muswada huo unapendekeza kila mtu, taasisi, shirika au kampuni binafsi inayokusudia kukusanya takwimu nchini ni lazima ipate kibali cha Serikali kabla ya kuzichapisha.

“Benki ya Dunia inafuatilia mwenendo wa haki na uhuru wa kujieleza katika takwimu nchini Tanzania,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Benki ya Dunia.