Binti wa kidato cha sita abakwa, anyongwa hadi kufa Iringa

Muktasari:

  • Lakini, ndoto hizo zimezimika ghafla baada ya mwanafunzi huyo wa Shule ya Sekondari ya Mwembetogwa kubakwa na watu wasiojulikana kisha kunyongwa hadi kufa.

 Sundi George alikuwa amebakiza siku 50 tu kabla ya kufanya mtihani wake wa taifa wa kidato cha sita.

Lakini, ndoto hizo zimezimika ghafla baada ya mwanafunzi huyo wa Shule ya Sekondari ya Mwembetogwa kubakwa na watu wasiojulikana kisha kunyongwa hadi kufa.

Mwanafunzi huyo alitakiwa kuungana na wenzake katika mtihani wa mwisho wa kidato cha sita itakayoanza Mei 7.

Taarifa za awali kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire zilieleza kuwa kifo hicho kilitokea Machi 12, na tayari watu wawili wanashikiliwa wakihusishwa na mauaji hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuna dalili kwamba rafiki yake wa kiume alihusika kwenye tukio hilo kwa kuwa tangu litokee hajaonekana.

“Binti huyu aliyebakwa licha ya changamoto hizi za mvua alikuwa mkavu, nguo hazikuloa na alitoweka usiku huo na wazazi hawakushtuka kabisa,” alisema Kasesela.

Akizungumza jana, mwalimu wa shule hiyo, Baraza Ramadhani alisema kifo hicho kimewasikitisha kwa sababu walitarajia angekuwa kati ya wasichana ambao wangefanya vizuri mitihani yao.

“Huyu binti alikuwa na akili sana na tulitegemea angepata daraja la pili hata la kwanza. Tumeumia kupita kiasi na kwa kweli inasikitisha,” alisema.

Ramadhani alisema siku moja kabla mwili wake kukutwa porini, mwanafunzi huyo alihudhuria masomo yake hadi saa 11 jioni.

“Huwa tuna madarasa ya ziada kwa wale wanaofanya mitihani kwa hiyo Sundi alikuwepo darasani na kwa sababu tuliwawekea utaratibu wa kusaini mahudhurio, alifanya hivyo,” alisema.

Alisema siku ya pili, walianza kusikia tetesi za kuwapo kwa mwanafunzi aliyeuawa na mwili wake kutupwa kichakani huku ukiwa na sare za shule.

Mwalimu Baraza ambaye pia ni katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Iringa alisema taarifa hizo ziliufanya uongozi kufuatilia na kubaini kuwa alikuwa ameshauawa.

“Niombe vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza tukio hili la kinyama ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua. Inaumiza mno kuona binti anauawa kikatili kabla hata ya kutimiza ndoto zake,” alisema.

“Kiukweli kijana huyu alikuwa mtulivu na mwenye heshima na tunashindwa kabisa kuelewa kwa nini mauaji haya yamemtokea.”

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwembetogwa, Monica Kafumu alisema bado wapo kwenye kitendawili kikubwa kisicho na majibu shuleni hapo kutokana na tukio hilo la kinyama.

Kafumu alisema anaamini kitateguliwa pale jeshi la polisi watakapotoa ripoti ya uchunguzi wa nani amehusika na sababu zilizofanya watekeleze mauaji hayo.

“Ni msiba mzito, tukio la kushtusha na kwa kweli hatuelewi imekuwaje? Huyu binti amewakosea nini? Ni laana kubwa kukatisha uhai wa binti mdogo kama huyu mwenye matarajio mengi ya maisha yake,” alisema.

Alisema tayari mwili wa mwanafunzi huyo ulishasafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani Mwanza na kwamba ameshazikwa.