Bodaboda zazidi kuua

Waendesha pikipiki wakipita katika makutano ya Barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Mataa ya Tazara, jijini Dar es Salaam.Picha ya Maktaba.

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha kuwa bodaboda huchukua maisha ya Watanzania watatu kati ya 17 kila siku.

Dar es Salaam. Usafiri wa bodaboda ambao umeanza miaka ya hivi karibuni sasa unaonekana kuchukua maisha ya watu wengi.

Takwimu zinaonyesha kuwa bodaboda huchukua maisha ya Watanzania watatu kati ya 17 kila siku.

Ndani ya miaka mitano  ajali za magari na bodaboda kwa ujumla zimesababisha vifo vya watu 30,783 na kujeruhi wengine 141,740.

Miongoni mwa vifo hivyo, 5,518 vimesababishwa na bodaboda pekee.

Takwimu hizo zilizotolewa jana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga zinaonyesha kuwa miongoni mwa majeruhi wa ajali hizo zilizotokea kuanzia Januari 2010 hadi Septemba mwaka huu, watu 28,341 walikuwa wa pikipiki hizo za kubeba abiria ambazo pia zilisababisha jumla ya ajali 29,136 ikiwa ni zile zilizoripotiwa polisi.