CCM yaitaka Takukuru kuwapigania wakulima wa pamba

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeingilia kati suala la wakulima wa pamba mkoani Morogoro ambao waliuziwa pembejeo na mzabuni, kwa kuitaka Takukuru kuchunguza jinsi alivyopatikana

Morogoro. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza taratibu zote zilizotumika kumpata zabuni aliyesambaza pembejeo kwa wakulima wa pamba.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu Novemba 5, 2018 na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogerei wakati akizungumza na Mwananchi ambapo ameitaka Takukuru mkoani humo kuchunguza ubora wa mbegu zilizosambazwa kwa wakulima wa wilaya ya Kilosa, Kilombero, Morogoro na Gairo kupitia mzabuni huyo. 

“Ninaitaka Takukuru iingilie kati ili kuchunguza mchakato wote uliotumika kumpata huyu mzabuni ili kama kuna vitendo vya rushwa vilifanyika basi wote waliohusika na uhuni huu akiwemo mzabuni huyo wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema Kalogeresi.

Ametaja hatua ambazo chama kinapendekeza kuchuliwa kwa mzabuni huyo endapo ataonekana kaleta udanganyifu ni pamoja na kurudisha gharama za wakulima waliopata hasara kutokana na kuuziwa mbegu na pembejeo zisizokuwa na ubora.

Naye mkuu wa wilaya ya Kilosa, Adamu Mgoyi amesema zao la pamba ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati hivyo msimu wa kilimo uliopita ulifanikiwa kuhamasisha wakulima wengi kulima pamba hata hivyo wakulima walipata hasara kutokana na pamba kukosa ubora.

Mgoyi amesema katika msimu wa kilimo uliopita, jumla ya heka 4,050 zililimwa pamba katika wilaya ya Kilosa lakini kutokana na hasara iliyopatikana, wakulima wameingia hofu hivyo yeye na wataalamu wake wa kilimo watakuwa na kazi kubwa ya kutoa tena hamasa ya kulima zao hilo.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amesema mkoa huo una jumla ya hekta 2.2 milioni zinazofaa kwa kilimo hata hivyo ni hekta 7,000 tu ndizo zinazolimwa.

Mkuu huyo wa mkoa, ameahidi kuwafuatilia wote waliohusika kusambaza pembejeo zisizofaa na kuwataka wakulima kutovunjika moyo na hasara waliyoipata badala yake waongeze hamasa ya kulima mazao yanayostawi katika maeneo yao.