13 wajeruhiwa ajali ya basi Masasi, dereva akikwepa shimo katikati ya barabara

Wananchi wakiangalia gari lilipinduka wilayani Masasi na kusababisha watu 13 kujeruhiwa.

Muktasari:

 Chanzo cha ajali iliyosababisha majeruhi 13 Masasi kimetajwa kuwa uwapo wa shimo kubwa katikati ya barabara, ambapo dereva alipojaribu kulikwepa spring ya kushoto ya gari ikakatika na kusababisha lipinduke.

Mtwara. Watu 13 wamejeruhiwa kwenye ajali ya basi iliyotokea leo Mei 5, 2025 Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara ikihusisha basi lenye namba za usajili T283 DZR linalofanya safari zake kati ya Mtwara na Mbeya.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, huku akieleza kwamba majeruhi hao 13 wanapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Masasi ya Mkomaindo.

Kamanda Suleiman amesema chanzo cha ajali hiyo ni shimo kubwa lililopo katikati ya barabara ambapo wakati dereva anajaribu kulikwepa, basi lilikatika spring na kupinduka.

“Hili basi lilikuwa linatoka Mkoa wa Mtwara kwenda Mkoa wa Mbeya, baada ya kufika Masasi, kilomita tano kutoka kituo cha mabasi, likaingia mtaroni baada ya kukatika spring, baadaye likaanguka. Hadi sasa, zaidi ya majeruhi 13 wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Masasi Mkomaindo,” amesema Sulaiman.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati wa Usalama Barabarani (RSA) Wilaya Masasi, Arif Lardhi amesema shimo lililopo katika barabara hiyo ni kubwa, hivyo wakati dereva akijaribu kulikwepa spring ya kushoto ilikatika na kusababisha gari hilo kupinduka.

“Barabarani kuna shimo, dereva alipokuwa analikwepa akavunja spring ya kushoto na gari likapinduka ambapo watu 13 wameumia na wamepelekwa hospitali, hali zao sio mbaya sana, wapo walipata mikwaruzo na wengine mshituko.

“Katika ajali hiyo, dereva pia ameathirika kwa kuwa alipata mshituko lakini wote wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Mkomaindo. Athari kubwa ni uharibifu wa chombo kutokana na barabara kuwa mbaya na mashimo, hivyo kusababisha gari kuacha njia,” amesema Lardhi.

Naye Said Malindi, RSA Masasi, amesema,  “tunachoshukuru hakuna aliyekufa lakini wapo majeruhi ambao wamewahishwa hospitali kwa ajili ya matibabu na wanaendelea vizuri kwa sasa, jitihada zinazofanyika ni kuhakikiaha gari imetoka shimoni imerejea barabarani,” amesema Malindi.