CCM Moshi yamtema katibu wa Uchumi na Fedha

Muktasari:

  • Mbali na kumvua madaraka hayo, lakini chama hicho kimemwagiza kiongozi wake huyo kurejesha eneo ambalo tayari amejenga nyumba ya kuishi, kwa madai ya kuvunja makubaliano baina yao.

Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM), Moshi mjini kimemvua madaraka katibu wake wa Uchumi na Fedha kata ya Karanga, Silas Mmbwambo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Mbali na kumvua madaraka hayo, lakini chama hicho kimemwagiza kiongozi wake huyo kurejesha eneo ambalo tayari amejenga nyumba ya kuishi, kwa madai ya kuvunja makubaliano baina yao.

Maagizo hayo yalitolewa jana na Katibu wa CCM wilaya ya kichama ya Moshi mjini, Loth Ole Nesele na kuridhiwa kwa kauli moja na wajumbe wa Halmashauri kuu ya kata hiyo.

Akijitetea katika kikao hicho Mmbwambo alisema hana kipingamizi cha kuvuliwa madaraka, lakini akasema CCM ndiyo waliovunja mkataba ambao ulimfanya ashindwe kutekeleza makubaliano hayo.