CRDB: Elimu ya fedha itamkomboa mtoto wa Afrika

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk Charles Kimei 

Muktasari:

Ili kufanikisha hilo, benki hiyo imepunguza kiwango kinachohitajika kumfungulia mtoto akaunti ili kumjengea utamaduni wa kuweka akiba.

Dodoma. Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Benki ya CRDB imewataka wazazi kuwajengea watoto wao msingi imara wa uchumi wa kujitegemea kwa kuwafundisha kuweka akiba.

Ili kufanikisha hilo, benki hiyo imepunguza kiwango kinachohitajika kumfungulia mtoto akaunti ili kumjengea utamaduni wa kuweka akiba.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dk Charles Kimei amesema leo Ijumaa, mkoani hapa kuwa wamefanya hivyo ili kutoa fursa hiyo kwa watoto wengi zaidi kupata huduma za benki.

“Akaunti inaweza kufunguliwa kwa Sh5, 000 badala ya Sh20, 000 inayokubalika kila siku,” amesema.

Amesema ili kujenga taifa imara linalojitegemea hapo baadaye, watoto wanahitaji elimu ya fedha hasa namna ya kuweka akiba itakayowasaidia kufanikisha ndoto zao walizojiwekea ndiyo maana ikaanzisha akaunti maalumu kwa ajili yao ijulikanayo kama Junior Jumbo.

Wakati ikitimiza miaka 20 sasa, benki hiyo inajivunia kwa kuwa na  ‘program’ za kutoa elimu kwa vijana na watoto ili kuongeza hamasa ya kila Mtanzania kumiliki akaunti na kutumia huduma nyingine za taasisi za fedha.

Kimei amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawajengea watoto wao uwezo wa kuelewa masuala ya fedha tangu wakiwa na umri mdogo ili kutopata changamoto wakiwa watu wazima.