Chadema yalia na Ma-DC, CCM yawajibu

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni katibu wa Baraza la Wazee Chadema, Roderick Lutembeka. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Wakati Chadema ikiwanyooshea vidole Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu na mwenzake wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole jana alizungumzia madai ya Irando kuwatambulisha madiwani watatu wa Chadema waliohamia CCM.

Dar/Kagera. Kitendo cha baadhi ya wakuu wa wilaya kupanda majukwaani kuwanadi wagombea wa CCM katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani, kimeendelea ‘kuchafua hali ya hewa’ baada ya Chadema kutaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua hatua.

Wakati Chadema ikiwanyooshea vidole Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu na mwenzake wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole jana alizungumzia madai ya Irando kuwatambulisha madiwani watatu wa Chadema waliohamia CCM.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema hata wakipeleka malalamiko kuhusu viongozi hao wa wilaya, hayasikilizwi.

“Tulipeleka malalamiko ya Buswelu kwenye Kamati ya Maadili ya Jimbo la Siha ambako mkuu wa wilaya hiyo anatuhumiwa kufanya kampeni na kutoa amri kwa polisi kuingilia kampeni za uchaguzi wa ubunge. Shida ni kwamba wenyeviti wa kamati hizo ni Das (Katibu Tawala wa Wilaya),” alisema Dk Mashinji.

Januari 21, katika uzinduzi wa kampeni za mgombea wa CCM Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel kwenye viwanja vya KKKT Karansi, Buswelu alipanda jukwaani na kusema Serikali haijaribiwi hivyo ni vyema kila mmoja akahakikisha anadumisha amani na kufanya siasa za kistaarabu katika kipindi chote cha kampeni.

Mkuu huyo wa wilaya alisema, Dk Mollel, ambaye awali alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema na kuhamia CCM ambako alipitishwa tena kuwania nafasi hiyo, ameleta heshima kwa wananchi wa Siha na kuwataka wananchi wote kumuunga mkono.

Juzi, Irando wa Wilaya ya Momba katika mkutano wa hadhara aliwatambulisha waliokuwa madiwani wa Chadema; Ayub Mlimba (Mwaka Kati), Simon Mbukwa (Kaloleni) na Amos Nzunda (Mpemba) ambao wamehamia CCM.

“Malalamiko yetu hayafanyiwi kazi kwa sababu kuna ugumu wa kiitifaki hapa. Das hawezi kumfungulia mashtaka bosi wake ambaye ni mkuu wa wilaya,” alisema Dk Mashinji.

Aliitaka NEC kuwa na muundo wake wa utendaji ambao hautegemei watumishi wa umma bali wawe na watumishi wao wenyewe kama ilivyo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Alibainisha kuwa walipeleka malalamiko NEC na kujibiwa kuwa imewaandikia barua wakuu wa wilaya na mikoa kuwataka kutoingilia uchaguzi mdogo kwenye maeneo yao.

“Tume inatakiwa kuwa kazini wakati wote na siyo wakati wa chaguzi pekee. Tume ina jukumu pia la kutoa elimu kwa wapigakura, kwa hiyo suala la kuwa na watumishi wake ni muhimu sana,” alisema Dk Mashinji.

Kuhusu Irando kuwatambulisha madiwani katika mkutano wa hadhara, Dk Mashinji alisema, “Tatizo lipo kwao, sio mpaka tuseme sisi. Yule mkuu wa wilaya anawatambulisha makada wa CCM. Hana tofauti na Buswelu na hayo ni maelekezo wanayopewa.”

Hata hivyo, siku ambayo Buswelu alimnadi Dk Mollel jukwaani Mwananchi lilizungumza na mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima aliyekiri kuwa halikuwa jambo sahihi.

Alisema vyama hivyo vinatakiwa kumshtaki katika Kamati ya Maadili inayoundwa na wajumbe wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi katika jimbo husika ndani ya saa 72 tangu kitendo hicho kilipotokea.

Alisema kamati ina mamlaka ya kuwasilisha suala hilo katika ngazi nyingine ya kisheria kama polisi au kwa DPP.

Polepole awajibu Chadema

Akizungumzia kitendo cha Irando kuwatambulisha madiwani waliohamia CCM, Polepole alisema si kweli na kubainisha kuwa mkutano wa mkuu huyo wa wilaya ulikuwa ni wa kujadili maendeleo ya wilaya hiyo.

Alisema madiwani hao walipokewa na kiongozi wa CCM aliyekuwa ameongozana naye kama kiongozi aliyefuatilia utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

“Siyo kweli kwamba mkuu wa wilaya amewatambulisha madiwani. Hadhara zote za umma zinazohusisha maendeleo kunakuwa na uwepo wa CCM ili kusimamia yale iliyoyaahidi,” alisema.

“Katika mkutano wa mkuu wa wilaya, wale madiwani walikwenda kwa ajili ya kutangaza kujivua uanachama wa Chadema.”

Alipoulizwa sababu za madiwani hao kukubaliwa kutambulishwa katika mkutano wa kujadili maendeleo badala ya kwenye ofisi za chama hicho alisema, “Umewapigia simu (CCM Momba) ukawauliza hilo swali? Ukiona umebanwa unachomokea popote, hata kwenye dirisha unatokea. Sasa wewe ulitakiwa uwaulize wao (madiwani) kwa nini walijitokeza pale.”

Alipoulizwa huenda jambo hilo limeandaliwa, alitaka swali hilo waulizwe madiwani husika, kwani anachokifahamu ni kuwa walikwenda kushiriki mkutano. “Wamekuja kwenye hadhara wanatangaza tunaachana na vyama vyetu, sasa ulitaka wazuiliwe?” alihoji Polepole.

Kuhusu kunadiwa kwa wagombea, Polepole alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa linafanyiwa uchunguzi na kamati ambayo hakuwa tayari kueleza ni kamati gani, lini imeanza na itakamilisha lini kazi hiyo.

Imeandikwa na Peter Elias na Kelvin Matandiko (Dar), Shaban Ndyamukama (Kagera).