Clinton aacha kilio bungeni Dodoma

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson

Muktasari:

Akizungumza baada ya kuwatambulisha wageni bungeni jana, Dk Tulia alisema walitarajia kwamba mambo yangeweza kuwa mazuri upande wao (wanawake) lakini haikuwezekana.

Dodoma. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema wabunge wanawake wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais wa Marekani, Hillary Clinton.

Akizungumza baada ya kuwatambulisha wageni bungeni jana, Dk Tulia alisema walitarajia kwamba mambo yangeweza kuwa mazuri upande wao (wanawake) lakini haikuwezekana.

“Safari hii haiwezekani, lakini asikate tamaa maana baada ya miaka minne mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi kuliko ilivyokuwa sasa. Nampa pole mama Clinton kwa kuwa safari hii haikuwezekana,” alisema huku wabunge wanawake wakigonga meza ishara ya kuunga mkono kauli hiyo.

Dk Tulia aliongeza, “Nasikia kuna watu hapa wanakwambia tungempeleka mheshimiwa fulani.., katika maeneo yale Mama Clinton angeshinda.”

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Marekani jana yaliteka hisia za wabunge wengi kwani kabla ya kuuliza swali lake kuhusu sekta ya afya, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo alisema ana masikitiko makubwa kwa sababu Clinton ameshindwa.

“Kwa niaba ya wanawake wenzangu, nampa pole Mama Clinton (kwa kushindwa katika uchaguzi). Tumeumia sana na tumerudi nyuma,” alisema.

Kauli hiyo ilimfanya Dk Tulia kumtaka Lyimo aeleze amepata wapi taarifa hiyo wakati bado (wabunge wanawake) wana faraja kuwa bado Clinton angeweza kushinda uchaguzi huo.

“Mheshimiwa Suzan umetoa wapi taarifa hizi wakati wengine bado tunajipa faraja kuwa bado anaweza kushinda,” alisema Dk Tulia na kwamba baada ya kupewa taarifa hizo ndipo alieleza kusikitishwa kwake kuanguka kwa mke huyo wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton.

Pia, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Khamis Kigwangalah kabla ya kujibu swali la Lyimo alianza kwa kumpa pole Clinton kwa kushindwa kwenye uchaguzi huo ambao mpinzani wake Donald Trump alishinda.

“Mimi ni balozi wa wanawake, ninawapenda sana wanawake lakini ninatoa pole sana kwa wanawake na ninampongeza Trump kwa ushindi alioupata,” alisema Dk Kigwangalah.