Takukuru yawahoji madiwani waliojiuzulu Arusha

Diwani wa kata ya Mbuguni wilayani Arumeru mkoani Arusha, Ahimidiwe Rico aliyerekodi sauti akishawishiwa ajiuzulu nafasi yake kulia akitoka nje ya ofisi za Takukuru mkoani Arusha mara baada ya kuhojiwa leo pembeni yake ni diwani aliyemsindikiza wa kata ya Nkoanenkoli, Wilson Nanyaro,picha na Moses Mashalla

Muktasari:

  • Baada ya kuhojiwa waliokuwa madiwani hawakutaka kuzungumza chochote wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.

Arusha. Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, wamewahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kuwa walipewa rushwa.

Waliofika Takukuru ni Catherine Mtui, aliyekuwa diwani wa viti maalumu, Japhet Jackson (aliyekuwa diwani wa Ambuleni) na Bryson Isangya (aliyekuwa diwani wa Maroroni). Baada ya kuhojiwa hawakutaka kuzungumza chochote wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.

Pamoja nao, diwani wa Mbuguni, Ahimidiwe Rico anayedaiwa kuwa ndiye alirekodi sauti na picha wakati akishawishiwa na viongozi wa Serikali na wa Halmashauri ya Meru amehojiwa kwa zaidi ya saa tatu leo Jumanne Oktoba 17, 2017.

Rico amesema amewaeleza Takukuru kila kitu ambacho anakifahamu katika sakata hilo, ikiwemo kuwarekodi viongozi ambao walimshawishi kujiuzuru udiwani.

"Msimamo wangu ni kwamba, nachukia rushwa. Nimewaeleza kila kitu na wao waliniuliza kuhusu vifaa nilivyotumia kuwarekodi nikawaambia ni mali ya mbunge, alivitoa nchini Uingereza," amesema.

Rico aliyesindikizwa na diwani wa  Nkwanankore, Wilson Nanyaro amesema  ana imani na Takukuru kwamba watafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.

 

"Nimewaeleza wazi kuwa hata shauri hili likienda mahakamani nipo tayari kwenda kutoa ushahidi na kuthibitisha sauti za watu ambao niliwarekodi," amesema.

Amesema baada ya mahojiano yaliyoanza saa tatu hadi saa sita mchana, maofisa wa Takukuru wamemwambia aondoke na watamuita watakapomuhitaji.

Hakuna ofisa wa Takukuru aliyekuwa tayari kuzungumzia mahojiano hao wakisema wasemaji ni makao makuu ya ofisi hiyo Dar yaliyoko jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, mbunge Nassari amekiri kumpatia vifaa vya kurekodi diwani Rico ili kufichua njama za kujiuzulu madiwani.