Nassari, Lema waitupia zigo Takukuru

Muktasari:

  • Wabunge hao wamesema hayo jana muda mfupi baada ya kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola.

Dar es Salaam. Wabunge wa Chadema, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) wamesema uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa unaowakabili waliokuwa madiwani wa Arusha na baadhi ya viongozi wa mkoa huo umeanza.

Wabunge hao wamesema hayo jana muda mfupi baada ya kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola.

“Tumepokewa vizuri sana na Kamishna wa Takukuru na timu yake... tumewapa ushahidi na wamesema wameshaanza kuufanyia kazi,” alisema Lema.

Alisema Mlowola amewahakikishia kuwa taasisi hiyo ni huru na wataufanyia kazi bila kujali kwamba umewasilishwa na upinzani.

Lema alisema Rais John Magufuli anapaswa kuliona hilo na kuchukua hatua ili uchunguzi uweze kufanyika vizuri huku Nassari akisema amemkabidhi Mlowola flash ya kile alichokisema jana Arusha na nyongeza na kusisitiza kwamba watatoa ushahidi zaidi.

“Tumesema tuna ushahidi, kama hawaamini na wakiendelea kujibu tutatoa zaidi ya hapa na mimi kesho nitakuja kufungua jalada hapa Takukuru,” alisema Nassari

Kuhusu mkanganyiko wa tarehe katika video yenye ushahidi, Nassari alisema: “Hiyo ni ‘setting’ tu lakini anayebisha aseme huyo si DC, si ofisi yake na wakibisha tutatoa ushahidi zaidi ya huu.”

Mchungaji Msigwa alisema kilichotokea Arusha kinafanana na Iringa.

“Nami nitakuja kuandika maelezo ya kilichotokea Iringa kwani ofisi ya mkuu wa mkoa na wilaya zinahusika,” alidai Msigwa.

Alipoulizwa kwa simu kuhusu ujio wa wabunge hao Mlowola alisema: ‘Nipo kikaoni, mtafute msemaji kwa suala hilo.”

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba alipotafutwa alisema, “Sipo ofisini, kwani nilikuwa safari, kesho nitakuwa ofisini hivyo nitaweza kuongelea hilo.”

Wabunge hao waliwasili Takukuru saa 8.39 mchana na ilipofika saa 10.04 jioni walitoka na kuzungumza na waandishi wa habari.

Wajibu mapigo

Wakati Lema na wenzake wakifanya hivyo Takukuru, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe alisema wamepata taarifa za ushahidi wa wabunge hao.

“Kama wametoa ushahidi na wameukabidhi Takukuru sasa waache vyombo vifanye kazi, lakini kinachoendelea sasa ni siasa za watu walioshindwa,” alisema

Alisema kimsingi CCM haina sababu yoyote ya kununua diwani kama ambavyo imedaiwa na wabunge hao.

Mbali ya Mdoe, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru, Timothy Mzava ambaye ameonekaa katika video hiyo, alisema  ameufuatilia ushahidi unaozungumzwa na wabunge hao na kubaini kuwa ni wa kuungaunga na hauna ukweli wowote.

Mzava alisema yeye ni mtawala na si mwanasiasa na hivyo hawezi kupangiwa majukumu ya kuwarubuni madiwani na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.

“Kama wanao ushahidi si wawape? Mimi majukumu yangu sio kuwarubuni madiwani mimi ni mtawala na sio mwanasiasa,” alisema Mzava.

Akizungumzia taarifa ya  kuagizwa na Mnyeti kusimamia harusi ya Bryson Isangya ambaye ni mmoja wa madiwani aliyejiuzulu,  Mzava alisema yeye hakuwa mshenga na endapo aliamua kushiriki harusi alishiriki kama ambavyo angefanya kwa harusi ya  mtu yeyote.

Katibu tawala huyo alisema kwa sasa anashauriana na mwanasheria wake kuangalia hatua za kuchukua kwa kuchafuliwa jina na siku chache zijazo atazungumza na waandishi wa habari.

Akizungumzia taarifa hiyo, Mnyeti alisema kwamba juzi alishindwa kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo kwa kuwa alikuwa ameenda hospitali kung’oa jino na hivyo bado anaendelea kupata matibabu.

Wakati Mnyeti ambaye jana ilielezwa kwenye mitandao kadhaa ya kijamii, kuwa angeongea na vyombo vya habari, hasa kutokana na kunukuliwa kwenye akauti ya Twitter yenye jina lake ikiahidi jana angezingumza lakini baadaye alisema hajatoa taarifa hiyo.

“Mimi bado napata matibabu ya jino nililong’oa juzi na siku chache zijazo nitazungumza na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo,” alisema

Diwani Isangya ambaye alitajwa kusaidiwa harusi yake aliyofunga wiki iliyopita alisema masuala ya ndoa ni mambo binafsi hivyo, asingependa kuyazungumza.