Utata askari Polisi akidaiwa kumjeruhi mtuhumiwa kwa risasi

Muktasari:

  • Inadaiwa ofisa huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) aliagiza mtuhumiwa atolewe mahabusu na alienda naye nyumbani kwake, akiwa na askari wengine wawili, ambako walimhoji huku wakifyatua risasi, na moja ikampiga kwenye paja.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Manyara limeingia lawamani baada ya ofisa wa kituo cha Mirerani wilayani Simanjiro kudaiwa kumpiga risasi mtuhumiwa wakati akihojiwa.

Mtuhumiwa anayetajwa kwa jina la Ronald Mbaga na wenzake wawili walikamatwa Machi 30, 2024 kwa tuhuma za kuiba bastola ya mfanyabiashara wa madini ambaye jina lake halijatajwa.

Inadaiwa ofisa huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) aliagiza mtuhumiwa atolewe mahabusu na alienda naye nyumbani kwake, akiwa na askari wengine wawili, ambako walimhoji huku wakifyatua risasi, na moja ikampiga kwenye paja.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi amekanusha mtuhumiwa kupigwa risasi, bali alichomwa kwa bisibisi akiwa katika mgodi wa Tanzanite, alipotuhumiwa kuiba madini, kabla hajakamatwa na Polisi.

“Hizo tuhuma tunazifanyia uchunguzi, lakini si sahihi kwa sababu hata huyo kijana anakana, yeye anachodai ni kwamba alipigwa na bisibisi akiwa kwenye mgodi huko Mirerani, kwa sababu wanafanya kazi mgodini.”

“Wakati yuko pale alikuwa anataka kuwapora mawe huko chini, kwa hiyo wakamchoma kwa bisibisi mguuni. Hata mzazi wake anakanusha anasema aliumia alipokuwa akifanya kazi kwenye mgodi,” amesema Katabazi.

Taarifa ambazo Mwananchi linazo ni kuwa tayari suala hilo limeshaanza kuchunguzwa na maofisa wa Polisi makao makuu, waliofika Mirerani wakiwa na maofisa wa Mkoa wa Manyara.

Juzi, Msemaji wa Polisi, David Misime alipotafutwa kwa simu alimtaka mwandishi atume ujumbe, hata alipotumiwa hakujibu na hadi tunakwenda mitamboni ujumbe huo haukuwa umejibiwa na simu haipokelewi.

Mbali na Polisi, taarifa zaidi zimeeleza kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Simanjiro pia imewahoji maofisa wa Polisi, akiwamo mkuu wa kituo.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala amekiri kuwa na taarifa za suala hilo, lakini akasema kwa sasa lipo chini ya mikono ya mamlaka za uchunguzi ili kubaini uhalisia wake.

Sababu za uchunguzi huo, Lulandala ameeleza ni uwepo wa taarifa kinzani kati ya kijana na Jeshi la Polisi.

"Kwa taarifa za awali kijana anasema amepigwa risasi, upande wa pili kwa Polisi wanasema hapana, kwa hiyo kuna ukinzani wa taarifa na majibu yataletwa na uchunguzi," amesema.

Kwa mujibu wa Lulandala, uchunguzi unaofanyika unahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari na Jeshi la Polisi.

"Kwa namna tukio lilivyo, kama kijana ni mhalifu kweli anaweza kusema amepigwa risasi, vivyo hivyo kwa Polisi nao wanaweza wakaamua kujitetea kwa hiyo uchunguzi ndiyo utakaotupa ukweli," amesisitiza.


Mashuhuda waeleza ilivyokuwa

Licha ya RPC Katabazi kukanusha madai ya kijana huyo kupigwa risasi, vyanzo vya ndani ya Polisi vimeeleza ilivyokuwa tangu Mbaga na wenzake walivyokamatwa Machi 30, 2024 na kukaa mahabusu hadi Aprili 20, 2024.

“Alikamatwa kwa tuhuma za kuiba bastola ya mtu mmoja hapo Mirerani ambaye pia ni mchimbaji wa madini,” kinaeleza chanzo cha habari.

“Ila wakati akiwa mahabusu, alichukuliwa na kupelekwa nyumbani kwa (anamtaja ofisa huyo wa polisi). Katika mahojiano na kumtesa, inasemekana alimpiga risasi,” kinaeleza chanzo hicho.

“Baada ya hapo (ofisa huyo) aliagiza mzazi wake aje amdhamini na kumchukua, lakini akampa sharti asionekane hapo Mirerani, vinginevyo watamuua. Inasemekana yule kijana alipewa Sh100,000 wakati anaondolewa pale,” kilisema  chanzo cha habari ndani ya Polisi.

Kilisema baba wa kijana huyo aliitwa na kuzungumza na maofisa wa polisi.

Askari mwingine wa kituo hicho (jina limehifadhiwa), pia alikuwa na maelezo kama hayo.

“Kweli bwana, dogo amepigwa chuma (risasi). Huyo mfanyabiashara ndiye analalamika kuwa amepoteza silaha, kwa hiyo akawa anamshuku yule kijana,” amesema.

Akimzungumzia mlalamikaji, askari huyo amedai amekuwa na tabia ya kuwapa fedha maofisa wa polisi ili wawanyanyase watu wasio na hatia.

“Inasemekana silaha yenyewe aliiweka rehani huko kwao, sasa akawa anashindwa kusema ukweli, akaamua kumsingizia yule kijana. Kwa hiyo alitoa fedha kwa polisi ili wambane yule kijana, kwa hiyo zile hela zikawa zinawachanganya,” amesema.

Taarifa zaidi zimedai mfanyabiashara huyo awali alitoa Sh1 milioni kwa baadhi ya maofisa wa polisi kituoni hapo na kuahidiwa kuongeza Sh5 milioni kama bastola ingepatikana.

“Ndiyo maana walikaa naye (kijana) mahabusu muda mrefu wakimbana ili hiyo hela ipatikane,” kilidai chanzo chetu.

Askari mwingine, amesema siku ya tukio walipelekwa vijana watatu, baada ya mfanyabiashara huyo kuwasilisha malalamiko.

“Basi wakawekwa ndani kesi ikawa inaendelea, (anamtaja ofisa huyo) si akamchukua yule kijana akaenda kumpiga risasi. Alimchukua yeye na vijana (askari) wake watatu na waliandikisha kwenye kitabu wakati wa kumtoa, lakini walipomrudisha akawa na majeraha mguuni,” amesema.

Amesema baada ya kumrudisha akiwa amejeruhiwa, walimwita daktari (hajatajwa jina) akamtibu majeraha.

“Kisha (ofisa huyo) akamlazimisha mmoja wa askari aandike sick (mgonjwa) kwenye kitabu, lakini yule askari akaandika good (hali nzuri),” amesema akizungumzia maelezo ya kwenye kitabu wakati mtuhumiwa aliporejeshwa mahabusu.

Chanzo chetu kimesema maofisa waliotoka Polisi Makao Makuu kupeleleza suala hilo waliwahoji askari waliokuwepo kaunta akiwemo aliyemtoa mtuhumiwa mahabusu.

Juhudi za kumpata kina Ronald Mbaga hazikufanikiwa ilielezwa alisafirishwa nje ya mkoa huo na amekuwa akirudishwa Mirerani na kuhojiwa kisha anaondoka.


Maelezo ya RPC

Kamanda Katabazi alipozungumza na Mwananchi, licha ya kukikiri kushikiliwa kwa Mbaga pamoja na wenzake, alikana kijana huyo kupigwa risasi.

“Ni kweli kuna silaha ilikuwa imepotea na ndipo (Mbaga) aliposhikiliwa, lakini hakuwa peke yake, kulikuwa na watuhumiwa wengi tu,” amesema.

Alipoulizwa kama kuna askari walioshikiliwa baada ya Mbaga kupigwa risasi, amesema:

“Ni mashahidi mbalimbali (wanahojiwa) kwa sababu tumefungua jalada la uchunguzi, ni watu mbalimbali kwenye hilo tukio kwa sababu hatujajua kama ni watuhumiwa au si watuhumiwa.”

Hata hivyo, amesema hakuna askari aliyeshikiliwa kwa malalamiko hayo.

“Tunachotafuta ni wale waliomchoma Mbaga kwa bisibisi,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu madai ya ofisa wa polisi kumpiga risasi Mbaga amesema:

“Mlalamikaji aliyefanyiwa ukatili anakataa, kwa hiyo ina utata. Yaani watu wanasema pembeni kwamba polisi wamefanya, lakini yeye anakataa.”

“Hata mimi nilimwita ofisini hakukuwa na vitisho vyovyote lakini mtu anaposema walimtisha hakuna ushahidi wa kumtisha. Mimi amekuja ofisini kwangu na nimemhoji kama kamanda amekataa,” amesema.

Alipoulizwa sababu ya kumweka mahabusu kwa wiki tatu amesema: “Hilo ni suala la kiupelelezi na kiutaalamu. Kuna makosa unaweza kujiuliza kwa nini unamshikilia mtu ndani, kwa hiyo ni suala la kiuchunguzi zaidi.

“Kwa mfano kama kuna tukio la mauaji au kuna tuhuma nyingine, tunaendelea kumshikilia na tunaendelea kuchunguza. Kwa hiyo kuna mambo ya kiuchunguzi siwezi kuyaongea sasa,” amesema.

Kamanda Katabazi amesema, “Kwa mfano kuna watu wengine wanakaa ndani kwa ajili ya mahojiano, mbona wengine hawasemi walikuwa na hofu. Tusiwe na hisia, aje mtu aseme kwamba imekuwa hivi na hivi, lakini tunaenda na hisia, tunachohitaji ni ushahidi.”

Alipoulizwa ni wakati gani Mbaga alichomwa bisibisi, amesema bado wanachunguza.

“Tunachunguza madai ya kuiba bastola na mambo ambayo anadai kwamba imekuwa hivi na hivi, hata kama ni askari wetu, lazima tulifanyie kazi. Ndiyo maana tunachukua wengine tunawakamata, si mara ya kwanza kukamata askari na wengine wako Magereza, wengine hatua za kinidhamu wengine mashtaka,” amesema


Baba mzazi akanusha

Mwananchi limezungumza na Francis Mbaga, baba mzazi wa kijana Ronald, naye amekanusha mwanawe kujeruhiwa kwa risasi, akasema ni mzima.

“Mbona ni mzima kabisa? Hamna, hayo ni mambo ya mitaani tu. Alishikiliwa polisi kwa mambo mengine tu, sasa hayo yanahusiana na nini?” amehoji.

Alipoulizwa sababu ya mwanaye kushikiliwa na Polisi, ameendelea kukanusha.

“Maneno ya mitaani bwana, achana nayo, ngoja kwanza niko busy kidogo,” amesema.