Dk Kigwangalla alikoroga Zanzibar, atoa ufafanuzi

Muktasari:

  • Simai alihoji uteuzi huo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea akitaka kujua ni sababu gani za msingi za waziri huyo kufanya uteuzi huo bila ya kuishirikisha Zanzibar.

Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu, Simai Mohamed Said amehoji uteuzi wa wajumbe wa kamati ya kitaifa ya kuandaa utambulisho wa Tanzania uliofanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla.

Simai alihoji uteuzi huo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea akitaka kujua ni sababu gani za msingi za waziri huyo kufanya uteuzi huo bila ya kuishirikisha Zanzibar.

Alisema kitendo cha Dk Kigwangalla kufanya uteuzi huo wiki iliyopita bila ya kushirikisha Zanzibar wala waziri husika ni ishara ya kuitenga Serikali ya Zanzibar pamoja na kuyapora madaraka ya waziri katika mambo mbalimbali ambayo ili kufanikiwa kwake ni lazima kuwe na ushirikiano baina ya pande hizo mbili za Muungano.

“Kamati ya awali ilikuwa haina hata Mzanzibari mmoja, lakini siku iliyofuata waziri huyo alitangaza kamati nyingine na kuwaingiza Wazanzibari watano jambo ambalo linaonekana kutoshirikisha Zanzibar katika uteuzi huo,” alisema Said.Kamati hizo ambazo mjumbe huyo ameonekana kuhoji ni kamati ya awali iliyotangazwa Desemba 8 yenye wajumbe 16, lakini Desemba 10 iliteuliwa ya pili ambayo imeongezwa wajumbe wengine watano wanaodaiwa kutoka Zanzibar.

Wajumbe hao watano ambao wanaungana na wenzao ni Javed Jefferj, Hafsa Hassan Mbamba, Miraji U. Ussi, Salim Alkhasas na Arafat Haji.

Kuhusu hilo, Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Rashid Ali Juma alisema kuwa Waziri Kigwangalla amefanya uteuzi kwa mujibu wa taratibu zake na kanuni za wizara zake na sheria ya utalii kama zinavyomuelekeza. Hata hivyo, alisema Serikali ya Zanzibar inazidi kuwasiliana na Dk Kigwangalla ili kamati zinazoundwa kama zinahusiana na Muungano wakae pamoja na kuwasilisha majina ambayo yatakuwa na uwiano katika kuziteua.

Lakini Dk Kigwangalla alitoa taarifa kuhusu uteuzi huo akisema, “Siku chache zilizopita mimi Hamisi Kigwangalla, katika kutekeleza majukumu yangu kama Waziri wa Maliasili na Utalii, niliteua kamati ya kitaalamu ya watu waliobobea kwenye mambo ya ubunifu wa mikakati ya masoko, mawasiliano, mahusiano kwa umma, utalii na biashara. Lengo kuu likiwa kuanzisha mchakato wa kitaalamu (technical) wa kuandaa utambulisho mpya wa Tanzania kwenye masoko ya kimataifa ya utalii.”

Alisema kamati hiyo inakusudiwa kufanya uchambuzi wa kina wa tafiti mbalimbali na kukusanya maoni kwa wadau mbalimbali muhimu kisha kumpelekea mapendekezo.

“Kwa kuzingatia ukweli kwamba, Maliasili na Utalii siyo wizara ya Muungano na kwamba utalii, kimsingi ni katika mambo yatakayodumisha zaidi Muungano wetu na umoja wetu, sababu kimkakati na kiutekelezaji hatuwezi kukwepana na kwamba uuzaji wa vivutio vya utalii ni katika mambo ya kufanywa kwa pamoja ili kuwa na tija kwa Taifa letu, nilipokea ushauri kwamba ni vyema tangu hatua za awali tuweke wajumbe wanaotokea Zanzibar, kwenye kamati hii.”

Alisema awali, walikuwa na fikra kwamba baada ya kazi za mwanzo kufanyika na kuwa na andiko la kitaalamu la kufanyia kazi, wangeanzisha mawasiliano rasmi ndani ya Serikali mbili, ambako kungekuwa na majadiliano ngazi ya wataalamu na baada ya hapo ngazi ya mawaziri.

“Tumekuwa na utamaduni wa kufanya kazi pamoja na kwa ukaribu kwenye kutangaza vivutio vilivyopo sehemu zote mbili za Muungano na tutaendelea kufanya hivyo. Watalii wanaokuja kwenye mbuga hupenda kwenda Zanzibar kufanya utalii wa fukwe, na wa kiutamaduni, na kinyume chake, hivyo hatuwezi kukwepa kufanya kazi pamoja.”

Alisema yeye ni muumini mkubwa na mahiri wa Muungano na utengamano kwa ujumla wake.

“Pia ni muumini mkubwa wa ushirikishwaji kama zana muhimu ya kufanyia maamuzi nyeti, siwezi kuwa wa kwanza kukiuka msingi wa imani yangu kama kiongozi. Hatua stahiki itakapofika tutakaa na waziri pacha wa utalii wa Zanzibar kushauriana na kukubaliana.”