Dk Kigwangalla aruhusiwa kutoka hospitali alikolazwa

Muktasari:

  • Arejea nyumbani baada ya kulazwa hospitalini tangu Agosti 4 alipopata ajali ya mkoani Manyara

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla leo ameruhusiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa na kwenda nyumbani.

Dk Kigwangalla ameruhusiwa baada ya jopo la madaktari bingwa wa Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) alikokuwa amelazwa  waziri huyo kujiridhisha kwamba afya yake imetengamaa na anaweza kurejea nyumbani na kwenda hospitalini hapo kama mgonjwa wa nje.

Jopo hilo la madaktari bingwa watano wa kada za mifupa, usingizi na magonjwa ya ndani limefikia uamuzi huo baada ya kumhudumia Dk Kigwangalla tangu Agosti 12 alipohamishiwa MOI kwa ajili ya matibabu ya kibingwa ya mkono wake wa kushoto baada ya awali kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Taarifa ya MOI iliyotolewa leo ilisema, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo,  Dk Respicious Boniface amemtakia kila kheri Dk Kigwangalla katika kutekeleza majukumu yake ya kitaifa kwani sasa anaweza kuendelea na majukumu yake ya kuwatumikia wananchi.

“Kwa niaba ya jumuiya ya Taasisi ya Mifupa MOI, tunakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako ya ujenzi wa Taifa.”

“Ilikuwa heshima kubwa kuwa nawe hapa kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja, tuna amini umeridhishwa na huduma zetu na kama kuna mahali umeona upungufu ni vyema ukatujulisha ili turekebishe,” alisema.

Dk Boniface alimweleza Dk Kigwangalla kwamba kwa kuwa yeye ni daktari itakua rahisi kubaini mabadiliko yoyote ambayo siyo ya kawaida na hivyo kushauriana na madaktari wa MOI ili kupata ufumbuzi.

Kwa upande wake, Dk. Kigwangalla ameushukuru uongozi wa MOI, madaktari na wauguzi ambao walikuwa wakimhudumia katika kipindi chote alipokuwa wodini.

“Nichukue fursa hii ya kipekee kuwashukuru watoa huduma, Watanzania wote ambao mmekua mkiniombea na kunitembelea hapa hospitali baada ya kupata ajali, namshukuru Mungu afya yangu inaendelea vizuri sasa na nimeruhusiwa kwenda nyumbani,” alisema.

Dk Kigwangalla alipata ajali ya gari Agosti 4 na kupata matibabu ya awali mkoni Manyara kabla ya kuhamishiwa katika Muhimbili na baadae MOI, ambapo katika ajali hiyo Ofisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba alifariki dunia.