Dk Mwakyembe atoa shukrani kwa Watanzania

Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo, Sanaa na Burudani, Dk Harrison Mwakyembe 

Muktasari:

Mwakyembe pia amewashukuru viongozi wote wa dini akiwamo Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zuberi pamoja na maaskofu.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo, Sanaa na Burudani, Dk Harrison Mwakyembe amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kuombeleza kifo cha mkewe Linah Mwakyembe kilichotokea usiku wa Julai 15 mwaka huu kwenye Hospitali ya Aga Khan.

Dk Mwakyembe pia amemshukuru Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa mchango mkubwa walioutoa katika kumuuguza mkewe.

Dk Mwakyembe ametoa shukrani hizo leo Julai 26 wakati akizungumza na wanahabari nyumbani kwake Kunduchi wilayani Kinondoni.

Mbali na hao, Dk Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela Mkoani Mbeya, amewashukuru viongozi wote wa dini akiwamo Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zuberi na maaskofu.

"Wanafamilia tutakumbuka moyo adhimu na upendo na ushirikiano tulioupata kutoka Katibu Mkuu wa wizara hii Profesa Elisante Ole Gabriel na viongozi wengine waandamizi wa Serikali. Mwisho kabisa Wanakyela kwa uvumilivu wao katika kipindi hiki kigumu," amesema Dk Mwakyembe.