Dk Slaa awapa wapinzani mbinu kwa Rais Magufuli

Muktasari:

  • Kadhalika, Dk Slaa, ambaye alikuwa katibu mkuu wa Chadema, amesema kabla vyama hivyo vya upinzani kulalamika, vinapaswa kutumia sheria kupata haki zao kama yeye alivyofanya mwaka 2011.

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amewapa wapinzani nchini, mbinu za jinsi ya kukabiliana na changamoto za kisiasa zinazowakabili, badala ya kulalamika.

Kadhalika, Dk Slaa, ambaye alikuwa katibu mkuu wa Chadema, amesema kabla vyama hivyo vya upinzani kulalamika, vinapaswa kutumia sheria kupata haki zao kama yeye alivyofanya mwaka 2011.

Akizungumza kwa njia ya simu katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Dk Slaa ambaye alitangaza kuachana na siasa za vyama muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema badala ya wapinzani kulalamika wanaweza kutumia sheria zilizopo ili kupata haki ya jambo lolote ambalo wanahisi wanaonewa au haliendi sawa.

Kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimekuwa vikitoa malalamiko yao kwamba vinaminywa na kutopatiwa haki huku wakitoa mifano ya kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara na kunyimwa haki ya kuandamana.

“Wamelalalamika kwa muda mrefu na mara kadhaa nimekuwa nikishauri hili. Narudia, tutafakari. Si muda wa kulalamika tena sasa ni kuchukua hatua,” alisema Dk Slaa aliyewahi kuwa mbunge wa Karatu kwa tiketi ya Chadema.

“Nionyesheni ni wapi sheria au kanuni yoyote inakataza kufanya mikutano au maandamano? Nionyesheni ni wapi tamko la Rais linaweza kufuta sheria zilizopo? Mimi ni mwanasheria, najua maana ya sheria. Hayo yote ni matamko tu. Rais hawezi kufuta sheria kwa tamko.”

Dk Slaa alisema wapinzani wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kutumia sheria kuhakikisha wanapata haki zao kama wanaamini kuwa zinaminywa.

“Wanaweza kutumia sheria ya The Basic Right and Judgment (Sheria ya Haki za Msingi na Hukumu) ya mwaka 1994 kufungua kesi mahakamani wamshtaki Rais au kiongozi yeyote ambaye wanaamini hawatendei haki, kuacha kufanya hivyo,” alisema.

“Lengo la sheria hii ni kuhakikisha inatoa haki kwa yeyote au kiongozi yeyote, akiwamo Rais ambaye anaonekana ama hatendi au kuminya kwa haki zake za msingi, unapaswa kwenda mahakamani na kutafsiri sheria hiyo.”

Dk Slaa alisema si vizuri wanasiasa wakalalamika tu bila kuchukua hatua wakati sheria zipo.

Dk Slaa alisema wakati akiwa mbunge, alikuwa akibughudhiwa na Jeshi la Polisi mara kwa mara, akikamatwa na kufikishwa mahamani bila sababu za msingi, lakini alipogundua kuwa anaweza kwenda mahakamani kuomba tafsiri hiyo, alichukua hatua.

“Mwaka 2011 nilitumia sheria hiyo, nikafungua kesi mahakamani. Chini ya sheria hii kesi inabidi kusikilizwa chini ya majaji watatu na mwaka 2013 nilishinda. Toka pale sikushtakiwa tena,” alisema.

Alitoa mfano mwingine wa mwaka 2002 wakati akiwa mbunge wa Karatu. alisema wakati huo Rais aliyekuwapo alitaka kuifuta Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, lakini yeye (Dk Slaa) alishirikiana na madiwani kufungua kesi ya kupinga isifutwe, jambo lililompa hofu hata jaji aliyekuwapo.

“Tulifungua kesi dhidi ya Rais aliyekuwapo, lakini baadaye kesi ile ilifutwa kwa kuwa ilionekana tunawaaibisha. Mimi si mtu wa kulalamika, nawasihi hata wao wasilalamike wafuate njia sahihi,” alisema.

Katibu huyo mkuu wa zamani wa Chadema aliwashangaa viongozi wa upinzani kuacha haki yao ikandamizwe ilhali walishawahi kwenda mahakamani mara kadhaa katika kesi mbalimbali na nyingi ziliisha kwa wao kushinda.

“Kinachonishangaza na sina jibu mpaka sasa kwa nini hili linawashinda sasa, hasa ukizingatia hivi sasa vyama vina mawakili na wapenzi wengi tofauti na ilivyokuwa awali? Mimi nilishinda kipindi ambacho hakuna mawakili wengi, kwa nini wao wanaendelea kulalamika?

“Kama kweli wana nia ya dhati ya kutaka Rais au kiongozi yeyote asiendelee kuwabughudhi, wachukue hatua mapema.”

Dk Slaa alisema siasa peke yake yake haisaidii na badala yake lazima ifanywe kwa misingi ya sheria ingawa alikubali kuwa kuna sheria nyingi nzuri ambazo hazisimamiwi.

Hata hivyo, alisema kinachotokea sasa ni nguvu aliyonayo Rais John Magufuli katika kutekeleza mambo mbalimbali, kama sheria ambazo awali zilikuwa hazitekelezwi.

“Tulikuwa na viongozi dhaifu lakini sasa Rais Magufuli amekuja, ameamua kusimamia sheria zote ndiyo tunalalamika. Mfano kulikuwa na Sheria ya Polisi, lakini ilikuwa haitekelezwi. Sasa amepatkana mwenye kauli inatekelezwa, lakini watu wanalalamika,” alisema.

Madai ya usaliti

Dk Slaa, ambaye aliondoka Chadema katika kipindi muhimu cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, anasema uamuzi wake si usaliti na kwamba tuhuma dhidi yake hazina mashiko.

“Mengi yamesemwa, lakini nikwambie tu huo ni upotoshaji mkubwa na kwamba mimi hilo halinisumbui. Ningeumia endapo kama kitu kinachozungumzwa kina ukweli,” alisema.

Alisema yeye ni “yuleyule na atabaki kuwa yuleyule” ambaye hoja yake ni mapambano dhidi ya ufisadi na hatanyamaza katika hilo.

Alisisitiza kuwa, kutokana na tuhuma hizo, aliamua kuandika kitabu ambacho kilikamilika February 2017 na sasa kiko katika hatua za mwisho za uchapishaji kabla ya kukizindua rasmi.

Dk Slaa alisema kitabu hicho kitakuwa na majibu yote ikiwamo tuhuma za usaliti.

“Watanzania wajiulize wako wapi sasa wale waliobadili gia angani, niwaambie tu Dk Slaa wa mwaka 1995 aliyekuwa akipinga ufisadi mpaka 2015 alipoachana na siasa vya vyama ni yuleyule, sijawahi kubadilika wala kuwa msaliti,” alisema.

“Hao wanaosema mimi msaliti waniletee ushahidi na nakwambia kama kuna yeyote ambaye atafanikisha kuleta hata nukta, nipo tayari kula matapishi yangu.”

Dk Slaa, ambaye baada ya kuachana na siasa aliamua kwenda kuishi nchini Canada, aliwashangaa wanaohusisha kukubali uteuzi wa kuwa balozi na usaliti.

Alisema wanaohusisha vitu hivyo viwili hawajui majukumu ya balozi kwa kuwa hayana uhusiano na siasa.

Alisema yeye kama balozi ni kweli yupo serikalini, lakini majukumu yake ni tofauti na viongozi wengine wa Serikali.

“Balozi ni mwakilishi wa Rais kwa mkuu wa nchi nyingine, pale unakwenda kwa ajili ya masilahi ya Taifa, hivyo siendi pale kwa ajili ya kuiwakilisha CCM au Chadema,” alisema.

Alisema anachosimamia kwa sasa ni sera ya nchi ambayo ilipitishwa wakati yeye akiwa mbunge na kuwa hata Rais Magufuli anatekeleza kitu ambacho kilishapitishwa wakati huo na ambacho hakikutekelezwa.

Alisema wajibu wake ni kudumisha na kukuza uchumi na siasa baina ya nchi hizo mbili.

Mwanasiasa huyo alisema wakati wote akiwa mbunge alikuwa akifanya kazi za kitaifa na ndiyo sababu katika uongozi wake hakuwahi kusikika akiomba fedha za ujenzi wa miundombinu kama barabara, maji au zahanati.

Alisema badala yake alifanya kazi za kitaifa na kuomba fedha za maendeleo ya jimbo lake kutoka kwa wafadhili.

“Tangu 1995 nilipeleka maendeleo jimboni kwangu bila kutegemea fedha za Serikali, sasa leo itanishinda nini kwa wadhifa nilionao kutafuta watalii waje nyumbani ili tukuze uchumi, kutafuta wawekezaji ili kuwekeza na kuongeza ajira ili pato letu liongezeke,” alisema.

“Sijaanza leo kazi hii, nilianza Karatu na matunda yangu yanaonekana ndiyo maana leo Karatu ni tofauti na majimbo mengine.”