Friday, September 14, 2018

Dulla mbavu jela miaka 30 kwa unyang’anyi

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi Hjumanne@mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Abdallah Shaha(32) maarufu Dulla Mbavu, baada ya kupatikana na hatia ya unyang'anyi wa kutumia silaha.

Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 14, 2018 na Hakimu Mkazi,  Flora Mjaya baada ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi kufunga ushahidi wao.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mjaya amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa.

Hakimu Mjaya amesema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo upande wa mashtaka uliwasilisha  mashahidi watano ambao wamethibitisha shitaka hilo pasi kuacha shaka.

"Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, hivyo basi utatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine kwenye tabia kama hii," amesema Hakimu Mjaya.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Sylvia Mitanto aliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia hizo.

"Mheshimiwa hakimu naomba Mahakama yako itoe adhabu kali  kwa Shaha ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye  tabia mbaya kama hii, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya unyang'anyi katika jamii,” amedai Mitanto.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilimpa nafasi Shaha ya kujitetea kwanini asipewe adhabu, kudai kuwa  anafamilia inayomtegemea hivyo anaomba kupunguziwa adhabu.

Katika hati ya mashtaka, mshtakiwa alitenda  kosa hilo Mei 16, 2017, eneo la Chanika wilayani Ilala.

Siku hiyo ya tukio, Shaha aliiba Sh 4.5milioni, kompyuta mpakato aina ya Toshiba yenye thamani ya Sh 850,000, pampu ya maji ya  Sh 500,000, simu mbili zenye thamani ya Sh 495,000.

Pia anadaiwa kuiba hereni za silva zenye thamani ya Sh 60,000, mkoba wenye  thamani ya Sh 45,000, vyote mali ya Twalibu Magasa.

Inadaiwa kiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, mshtakiwa alimtishia Magasa kwa panga ili aweze kujipatia vitu hivyo bila kikwazo.

-->