Hakimu ahoji uchunguzi kesi ya vigogo wa uthamini madini kutokamilika

Muktasari:

  • Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika jambo lililomshangaza Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri

Dar es Salaam.  Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi  inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika jambo lililomshangaza Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

 

Hayo yalielezwa leo Oktoba 22, 2018 na wakili wa Serikali, Tulia Helela mbele ya Mashauri, kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

 

Wakili Helela amedai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuomba shauri hilo lipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.

 

Baada ya kueleza hayo Hakimu Mashauri  alimueleza kuwa kesi hiyo ni ya zamani na jalada lilikuwa kwa DPP likapelekwa kwa DCI (Mkurugenzi wa Makosa ya Jina) na kurejeshwa tena kwa DPP, “Juni 18, mwaka huu hadi leo hamjui kwamba hamuwatendei haki washtakiwa.”

 

Hakimu Mashauri baada ya kueleza hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 5, 2018.

 

Washtakiwa  wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania  (Tansort),  Archard Kalugendo na mthamini almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu ambao ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini, wote walikuwepo mahakamani.

 

Kalugendo na Rweyemamu wanasota mahabusu kutokana na DPP kuzuia dhamana zao na wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni.

 

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh 2,486,397,982.54 ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

 

Washtakiwa hao wanadaiwa  kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa almasi wa Serikali na waajiriwa wa wizara hiyo waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 1,118,291.43  ambazo ni sawa na sh 2,486,397,982.54.

 

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo ya Kisutu  haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.