Halotel kuwekeza Sh1.5 trilioni sekta ya mawasiliano Tanzania

Muktasari:

Kampuni ya mtandao wa simu ya Halotel imeadhimisha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake hapa nchini kwa kujivunia kutoa huduma zilizo bora


Dar es Salaam. Kampuni ya mtandao wa simu ya Halotel inatarajia kuwekeza Dola 700 milioni za Marekani, katika sekta ya mawasiliano nchini.

Uwekezaji huo, unatarajia kuwezesha kampuni hiyo kuwafikia wateja zaidi ya milioni sita katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Hayo yalisema leo Oktoba 16, 2018 jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Halotel, Nguyen Van Son alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka mitatu ya kampuni tangu ilipoanzishwa nchini.

Son amesema wanakusudia kuendelea kuiboresha huduma ya mtandao huo katika eneo la pesa kwa njia ya mtandao ijulikanayo kama ‘Halopesa’ sambamba na kitengo cha teknolojia ya mawasiliano ‘ICT’ kwa ajili ya wateja wa mashirika binafsi na Serikali kwa ujumla.

Amesema wanapoadhimisha miaka mitatu, tayari Halotel imeshafanya uwekezaji unaofikia Dola 500 milioni  za Marekani ikiwa ndiyo kampuni inayoongoza kwa kuwekeza miundombinu ya mawasiliano sehemu mbalimbali nchini inayofikia asilimia 95 ya wananchi wote ikiwa ni vituo 4,400 vya kupokea mawasiliano kwa umbali wa kilomita 18,300.

“Halotel imelenga kuwafikia watu walioko pembezoni mwa miji kwa kuwapa gharama nafuu za mawasiliano huku ikiwa tayari imewafikia wananchi zaidi ya milioni tatu sambamba na milioni moja wengine waliojiunga na mtandao wa Halotesa,” amesema

Naibu mkurugenzi huyo amesema hivi karibuni, kampuni hiyo itawekeza kiasi cha Dola 200 milioni za Marekani kwa ajili ya kuboresha huduma za mtandao na zaidi kuhakikisha inaimarisha mtandao wa 4G kwa wateja  wake kote nchini.

Amesema kampuni hiyo inalenga kuwafikia wateja zaidi ya milioni sita pamoja na watumiaji milioni tatu wa huduma ya Halopesa baada ya miaka mitano kuanzia mwakani.