Hoja kinzani ahadi ya Sh50 milioni kwa kila kijiji

Muktasari:

  • Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wabunge wamesema walijua kuwa ahadi hiyo ni ngumu kutekelezeka huku wenyeviti wakisema wananchi wamesalitiwa.

Dar/mikoani. Siku moja baada ya makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (SSH) kusema ahadi ya Sh50 milioni kwa kila kijiji haitatekelezwa kwa sasa, wenyeviti wa vijiji, mitaa na wabunge wameipokea kauli hiyo kwa mtazamo tofauti.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wabunge wamesema walijua kuwa ahadi hiyo ni ngumu kutekelezeka huku wenyeviti wakisema wananchi wamesalitiwa.

Ahadi hiyo ya Sh50 milioni kila kijiji ipo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 iliyonadiwa na Rais John Magufuli alipokuwa mgombea katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Lakini juzi, Samia akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza, Kigoma alisema wananchi hawatapelekewa fedha hizo na badala yake zitakwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kuliko kutoa fedha hizo kwa kila kijiji, Serikali imeamua kuwekeza katika elimu, afya, barabara na maji lengo likiwa ni kupeleka maendeleo kwa wananchi. “Katika mipango yetu ya sasa hilo la Sh50 milioni tumeliweka pembeni kwanza,” aliongeza.

Wenyeviti watoa neno

Mwenyekiti wa Mtaa wa Msangalalee Mashariki katika Kata ya Dodoma Makulu katika jiji la Dodoma, William Chacha alisema, “Mimi sina wasiwasi kwa sababu aliyeziahidi ndiye aliyebadilisha matumizi kwa hiyo tusubiri tu,” alisema Chacha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Shirimatunda kilichopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Beda Massawe alisema ahadi ya kupeleka Sh50 milion kila kijiji ndiyo iliyofanya chama hicho kuingia madarakani na sasa kusitishwa ni sawa na kuwasaliti Watanzania.

Clemence Nkya, ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Shirinjoro kilichopo Wilaya ya Hai alisema ilani ya CCM ililenga kuwainua wananchi ambao ni wa kipato cha chini, hivyoanashangazwa na hatua ya usitishwaji wa fedha hizo.

Emmanuel Lesio mwenyeviti wa Kitongoji cha Maendeleo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha alisema bado wana imani na Serikali juu ya kutekeleza ahadi hiyo.

Walichosema wabunge

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema, “CCM hawawezi kutekeleza ahadi zao wenyewe na ni wakati wa wananchi kuwanyoosha kwa kuwakataa. Ahadi ni deni na CCM wameshindwa kutimiza ahadi.”

Mbunge wa Hanang’ (CCM) Dk Mary Nagu alisema kauli ya Makamu wa Rais haina shida kwani walikuwa katika sintofahamu juu ya matumizi ya fedha hizo na jambo hilo ni gumu kwenye utekelezaji.

“Mimi nimewahi kuwa waziri wa maendeleo ya wanawake na watoto, ninajua ulivyo ugumu wa matumizi ya fedha katika maeneo ya vijijini, zile fedha zisingekuwa na tija yoyote,” alisema Dk Nagu.

Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), Vedastus Ngombale alisema mpango wa milioni 50 kila kijiji ulikuwa ni ahadi hewa ambazo wamebaini utekelezaji wake ni mgumu kama ambavyo upinzani uliwahi kusema.

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya alisema kauli ya Makamu wa Rais imethibitisha CCM walikuwa wanatoa ahadi ambazo kwa vyovyote utekelezaji wake ulionekana kutowezekana.

“Huwezi kupindisha ukweli kwa namna yoyote ile, pale walidanganya na bora Makamu wa Rais amesimamia ukweli kwamba haiwezekani, sasa ngoja tuone watunge kingine tena,” alisema Bulaya. Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy alisema tangu mwanzo alikuwa akipinga jambo hilo na alijua kuwa iko siku ukweli utajulikana.

Imeandikwa na Habel Chidawali, (Dodoma), Happiness Tesha (Kigoma), Rachel Chibwete (Dodoma) na Ibrahim Yamola (Dar)

Wakati hayo yakiendelea, jana imebainika kuwa kuna baadhi watu wanatumia jina la Makamu wa Rais, Samia Suluhu kuwatapeli wananchi kwa kuwachangisha fedha ili wapate Sh50milioni.

Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Soweto, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Munzeze wilayani Buhigwe, Kigoma Mama Samia alisema baadhi ya watu wanapita vijijini na kuwachangisha wananchi fedha wakiwarubuni kuwa watapata Sh50 milioni.

“Huu ni uongo na hao ni matapeli wakamatwe mara moja,” alisema

Imeandikwa na Habel Chidawali, (Dodoma), Happiness Tesha (Kigoma), Rachel Chibwete(Dodoma) na Ibrahim Yamola(Dar)