JPM amtega tena mbunge wa upinzani Kigoma

Muktasari:

DONDOO

“Sasa hivi mnalalamika maji, kwani Mbunge wa hapa hakusema suala la maji atalimaliza? Leo amelimaliza? alihoji huku wananchi wakipiga kelele kuashiria “hapana”.

Rais Magufuli 

Dar/Kigoma. Rais John Magufuli ‘amemkaanga’ mbunge wa upinzani wa Jimbo la Buyungu, Kigoma huku akisema kuwa wananchi wa eneo hilo wanateseka kutokana na makosa ambayo waliyafanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akihutubia wananchi wa mkoa huo jana, wakati wa  ziara yake ya kikazi katika Ukanda wa Magharibi, Rais Magufuli alisema maendeleo yanaletwa na chama tawala (CCM) na kwamba wananchi walikosea kuchagua mbunge wa upinzani.

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mbunge wa Jimbo la Buyungu, Kasuku Bilago Samson (Chadema) kuelezea kuwa eneo hilo lina uhaba  mkubwa  wa maji.

“Kabla sijazungumza chochote naomba mbunge wa hapa awasalimu,” alisema Rais Magufuli ambaye alikuwa wilayani Kakonko kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi.

Mara baada ya kusimama, mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kueleza kero ya maji kwenye jimbo lake.

“Naomba niseme tunalo tatizo la maji katika Jimbo la Buyungu hususan Kakonko mjini,” alisema.

Licha ya ombi hilo kupokewa na Rais Magufuli, lakini ni kama mbunge huyo alikuwa amejikaanga kwa mafuta yake na mbele ya wapiga kura wake. Rais Magufuli alisema, “Nawashukuru sana kwa kuwa mlichagua wabunge wengi wa CCM. Hebu wabunge msimame wote pamoja na yule mmoja mwingine (Chadema),” alisema na kuongeza:

“Sasa hivi mnalalamika maji, kwani mbunge wa hapa hakusema suala la maji atalimaliza? Leo amelimaliza? alihoji huku wananchi wakipiga kelele kuashiria “hapana”.

“Sasa ndiyo muanze kujifunza kidogokidogo, lakini namshukuru kwa kuwa anatoa ushirikiano,” alisema Rais Magufuli.

 Hii ni mara ya pili kwa  Rais Magufuli kuwakaanga wabunge wa upinzani katika mikutano ya hadhara, kwani amewahi kumtaka mbunge wa Liwale (CUF), Vedasto Ngombale kuchangia Sh15 milioni za mfuko wa jimbo katika ujenzi wa kituo cha afya. Hata hivyo, Ngombale alisema hawezi kutoa fedha hizo kwa bajeti ya mwaka huu kwani alishapanga bajeti kwa kata zake 13.

Akiwa katika ziara mkoani Kigoma jana, Rais Magufuli aligusia uteuzi wa mawaziri wawili ambao wanatokea mkoa huo; Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

“Nilimwambia wewe ni Profesa(Ndalichako),nenda watakupa ubunge, akaniambia mimi sitapita. Lakini ni mchapakazi sana, nikaona nimteue tu kwenye nafasi yangu,” alisema alipozungumzia suala la ubora wa elimu.

“Nikamwambia na wewe (Dk Mpango) nenda ukagombee, akasema hawawezi kunipa, Kigoma huwa hawajali. Nilipopata urais nikamteua na nikampa uwaziri wa fedha,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa barabara Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa barabara hiyo ina urefu wa kilomita 50 kutoka Kibondo hadi Nyakanazi na itagharimu Sh48.7 bilioni zote kutoka serikalini.

Alisema mradi huo, utasaidia kufungua fursa za kiuchumi katika eneo hilo pamoja na kuziunganisha nchi jirani zikiwamo Burundi na Rwanda.

Rais Magufuli alimuagiza mkandarasi wa Kampuni ya Nyanza inayosimamia mradi huo, kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

“Kufukuza makandarasi kwangu ni kama kunywa chai, nataka barabara hii iishe na vifaa visiondoke hapa,” alisema Rais Magufuli ambaye amewahi kuwa Waziri wa Ujenzi.

Kodi Vituo vya Mafuta

Rais Magufuli hakuacha kuzungumzia ulipaji kodi na aliwashukia wafanyabiashara, hasa wamiliki wa vituo vya mafuta kwamba ni lazima walipe.

Alisema Serikali ilikuwa inakusanya kodi ya Sh800 bilioni kwa mwezi, lakini baada ya kuwabana imeongezeka hadi kufikia Sh1.2 trilioni. “Nafahamu wengi wanaokwepa kodi sio wananchi wa kawaida, ni wale matajiri wakubwa,” alisema na kuongeza:

“Lakini, wapo wanaokwenda kununua mafuta, umelipa kodi humohumo kwenye nauli ya mabasi ila wao hawataki kulipa kodi. Nitalala nao mbele, watazitema tu,” alisema.

Alisema ametoa siku 14 kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanalipia kupitia mashine za kielektroniki (EFD).

Hali ya chakula

Wakati akimalizia hotuba yake, Rais Magufuli alisema Serikali haitatoa chakula kwa wananchi licha ya kuwapo kwa uhaba wa chakula eneo hilo.

Alisema jukumu la Serikali ni kuboresha miundombinu pamoja na kutoa huduma muhimu ikiwamo elimu, barabara na umeme.

“Inawezekana wengine walidhani Rais anawaletea chakula, siwaletei chakula ng’oo!. Usipofanya kazi na usile na usipokula ufe. Ni lazima kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi na afanye kazi,” alisema. 

Baada ya kumaliza mkutano huo, Rais Magufuli alielekea Kasulu na njiani alilazimika kusimama kwa muda katika mji wa Kibondo ili kuongea na wananchi.

Wakati huohuo, Rais Magufuli alizungumzia suala la mafisadi na kwamba amejitoa bila kujali vitisho. “Nimekuwa mkali kwa mafisadi, nina watumbua bila aibu na nitaendelea kuwatumbua,”alisema huku akishangiliwa na wananchi. Pia, aliwataka wananchi hususan wakulima kutokubali kulipishwa kodi za usafirishaji wa mazao yaliyo chini ya tani moja baada ya kufutwa tozo zaidi ya 80 za kilimo.

Amega hifadhi, agawa kwa wananchi

Akiwa Kasulu, Rais Magufuli alitoa sehemu ya hifadhi ya msitu wa Makere Kusini uliopo wilayani humo kwa ajili ya kutumika kwa shughuli za kilimo na akawaonya wakulima kutovamia eneo jingine la hifadhi.

Alitoa eneo hilo la msitu alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Kasulu-Kidahwe yenye urefu wa kilomita 63 inayojengwa na Kampuni ya Chico kwa kiwango cha lami itakayogharimu shilingi66.3 bilioni.

“Najua ardhi ile ya hifadhi ina mbolea na rutuba ya kutosha ndio maana watu wanakwenda kulima huko na wanavuna mazao mengi, lakini natambua kwamba mmekuwa mkiingia kwa siri kulima na Serikali imekuwa ikiwaondoa,” alisema na kuongeza:

“Nimejiuliza sana tangu jana (juzi) kuhusu hili jambo, kwa vile nyie watu wa Kasulu ni wakulima wazuri nimeamua kutumia madaraka niliyonayo kuwapatia eneo mlilokuwa mnalima ili muendelee kulima, japo kuna sheria, lakini naamua kutumia ubinadamu kwenu,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kauli hiyo watu waliokusanyika katika mkutano huo walilipuka kwa shangwe na vifijo kwa zaidi ya dakika moja, jambo lililoashiria ni kufurahia uamuzi huo.