JPM auchambua udhaifu UVCCM

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli akihutubia alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Vijana wa CCM katika Ukumbi wa Julius Nyerere mjini Dodoma jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

Rais alisema hayo katika siku ambayo mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis alikuwa mahabusu baada ya kukamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutumia fedha kushawishi wapiga kura, huku mwanachama mpya, Albert Msando akieleza jinsi uongozi ulivyomdangany Rais kuhusu idadi ya wanachama wa jumuiya hiyo. Sadifa, ambaye pia ni mbunge wa Donge visiwani Zanzibar, alikamatwa nyumbani kwake eneo la Mailimbili mkoani Dodoma.

Mwenyekiti wa CCM, John Magufuli jana aliamua kuwaweka sawa wajumbe wa mkutano mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), akisema umekuwa dhaifu na kugubikwa na vitendo vya rushwa, ndio maana haukupendekeza majina ya kumwezesha kufanya uteuzi.

Rais alisema hayo katika siku ambayo mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis alikuwa mahabusu baada ya kukamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutumia fedha kushawishi wapiga kura, huku mwanachama mpya, Albert Msando akieleza jinsi uongozi ulivyomdangany Rais kuhusu idadi ya wanachama wa jumuiya hiyo. Sadifa, ambaye pia ni mbunge wa Donge visiwani Zanzibar, alikamatwa nyumbani kwake eneo la Mailimbili mkoani Dodoma.

Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kuhanga alisema watamfikisha mahakamani leo baada ya kukutwa akiwapa soda wajumbe wa UVCCM kutoka Kagera nyumbani kwake.

Alisema walikesha kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Akifungua mkutano huo, Rais Magufuli alisema amejifunza kwamba vijana wa CCM wapo na wanayaweza isipokuwa walipotezwa hivyo utendaji wao kupungua.

“Ninapozungumza hapa tu, pamoja na kwamba sitaki kuhukumu, mwenyekiti wenu wa Umoja wa Vijana yuko rumande kwa kushikwa na rushwa. Huo ndiyo umoja wa vijana tuliokuwa tunaenda nao,” alisema.

Alisema uelekeo ambao UVCCM ilikuwa ikienda siyo ambao anaujua kwa kuwa hata yeye aliwahi kuwa mwanachama wa umoja wa vijana, hivyo unatakiwa kufanyiwa marekebisho.

Rais Magufuli alisema alipoingia madarakani, UVCCM haikumpelekea orodha ya majina ili kumwezesha kuteua vijana kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali yake, hivyo alitumia mbinu zake kuwatambua.

Aliwataka wafanye mabadiliko kwenye umoja huo kwa kuchagua viongozi makini ambao watakuwa washauri wake.

“Mkichagua kama wale ambao hawakunishauri hata kwa kuniletea majina ya kuteua kwenye nafasi zenu, mjue mna miaka mitano mingine ya kuumia,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa.

“Nitashangaa kama mtaniletea mwenyekiti aliyewahonga. Kuwahonga ni dalili ya kuwamaliza thamani yenu. Kukupa hela ili umchague ni kama amekudharau na hii ni dalili ya mwanzo kuonyesha kuwa huyu hatakuwa kiongozi mzuri.”

Kuhusu mali za UVCCM, mwenyekiti huyo alisema zipo nyingi kama vile majengo lakini zinatumika hovyo. Alitoa mfano wa jengo la umoja huo lililopo Dar es Salaam ambalo haijulikani linakusanya mapato kiasi gani kila mwaka.

Alisema jumuiya hiyo ina viongozi ambao ikifika wakati wa uchaguzi wanawekwa mfukoni na wagombea.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema ni wakati wa bodi ya wadhamini ya UVCCM kuondoka kwa sababu haina msaada wowote kwa jumuiya hiyo.

Huku William Lukuvi ambaye pia ni waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi kama mmoja wa wajumbe wa bodi akimsikiliza, Magufuli alisema haiisaidii UVCCM.

Alisema hilo linawezekana kama wataamua kumfuata yeye, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu na kumweleza mpango wao naye akawasaidia.

“Viongozi mtakaochaguliwa, fanyeni tathmini ya mali za umoja wa vijana, zote ziwe kwenye daftari moja, zijulikane na mjue zinaingiza kiasi gani,” alisema.

Kabla ya Rais kuzungumza, wanachama wapya walipewa nafasi ya kuzungumza na wajumbe na aliyeshtua wengi alikuwa Msando, ambaye anatokea ACT-Wazalendo.

Msando alisema UVCCM haiwezi ikaongozwa na watu ambao hawajui hata idadi ya wanachama wao, akitoa mfano wa nyaraka mbili tofauti; moja ikionyesha umoja huo una wanachama milioni sita na nyingine ikionyesha ina wanachama milioni 1.1 walio hai na 400,000 ambao si hai.

Alisema takwimu hizo zinalenga kumpotosha Rais ajione ana vijana wengi kumbe idadi ni ndogo na akautaka umoja huo kufanya jitihada ya kuhakikisha unafufua wanachama na kuongeza wengine.

Msando, ambaye alijivua uanasheria wa ACT-Wazalendo baada ya video inayomuonyesha akimpapasa malkia wa video, Gigiman kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, alisema ni muhimu kwa viongozi wa umoja huo kujitambua.

Akielezea utendaji wa UVCCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, naibu katibu mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alisema kuna ongezeko la wanachama kutoka 233,506 mwaka 2008 – 2012 hadi kufikia 1.7 milioni.