JPM awajulia hali Ngosha, Shukuru

Muktasari:

Wagonjwa hao wamechukukua nafasi kwenye vyombo vya habari wiki hii. Mzee Ngosha aliibua mjadala baada ya kuenea kwa taarifa za kuugua kwake huku baadhi ya wananchi wakitaka Serikali kumuenzi kutokana na mchango wake kwa Taifa.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alikwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kumtembelea mzee anayeelezwa kuwa alibuni Ngao ya Taifa, Francis Kanyasu ‘Ngosha’ pamoja na mtoto ambaye amekuwa akiishi kwa kunywa mafuta ya kula, sukari na maziwa, Shukuru Kisonga.

Wagonjwa hao wamechukukua nafasi kwenye vyombo vya habari wiki hii. Mzee Ngosha aliibua mjadala baada ya kuenea kwa taarifa za kuugua kwake huku baadhi ya wananchi wakitaka Serikali kumuenzi kutokana na mchango wake kwa Taifa. Kwa mtoto Shukuru habari yake imekuwa ya kustaajabisha kutokana na kula mafuta ya kupikia, sukari kwa wingi na maziwa katika maisha yake jambo ambalo halikuwa la kawaida.

Rais Magufuli akiwa ameambatana na mkewe, Mama Janeth, aliwatembelea wagonjwa hao waliolazwa katika vyumba namba 310 na 312, ambako pia waliwapa pole wagonjwa wengine waliolazwa katika Wodi ya Mwaisela hospitalini hapo.

Akiwa wodini hapo, Rais Magufuli alizungumza na madaktari na wauguzi wa Muhimbili na kuwashukuru kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwahakikishia kwamba Serikali inazifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili wao pamoja na hospitali hiyo.

“...Mnafanya kazi nzuri, madaktari wote nchini pokeeni pongezi zangu, sisi Serikali tutaendelea kuzikabili changamoto hizo na siku moja zitakwisha, kikubwa ni kumtanguliza Mungu mnapofanya kazi ya kuokoa maisha ya watu.Mnafanya kazi ya Mungu,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu wagonjwa hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema tayari madaktari wameshagundua magonjwa yanayowakabili Mzee Ngosha na mtoto Shukuru na kwamba wanaendelea vizuri na matibabu.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi