Jela miaka 25, faini Sh3.7 bilioni

Mtuhumiwa wa kesi ya kusafirisha meno ya tembo yaliyokamatwa nchini Taiwan mwaka 2009, Michael Kijangwa (wa pili kutoka kushoto mstari wa mbele) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Tanga, jana. Picha na Picha na Burhani Yakub

Muktasari:

Meno hayo yenye thamani ya Sh247.5 milioni, yalikamatwa Novemba 2009 katika Bandari ya Koushug, Taiwan yakisafirishwa kuelekea Manila, Ufilipino yakiwa yametokea Bandari ya Tanga.

Tanga. Baada ya kusakwa tangu mwaka 2009 ili kujibu kesi iliyokuwa inamkabili ya kusafirisha meno ya tembo, Michael Kijangwa (57) alikamatwa jana na kusomewa hukumu iliyokuwa ikimsubiri tangu mwaka 2014 ambayo ni kwenda jela miaka 25 na kulipa faini ya Sh3.7 bilioni.

Meno hayo yenye thamani ya Sh247.5 milioni, yalikamatwa Novemba 2009 katika Bandari ya Koushug, Taiwan yakisafirishwa kuelekea Manila, Ufilipino yakiwa yametokea Bandari ya Tanga.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Cresencia Kisongo alisema Kijangwa alijinyima haki ya kutoa maelezo mahakamani hapo kutokana na kukimbia baada ya kupewa dhamana kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza Desemba 10, 2009.

“Ninachokifanya leo (jana) ni kutoa hukumu ambayo tayari ulishakuwa umehukumiwa mwaka 2014 baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka manne kati ya 17 yaliyowasilishwa mahakamani hapa,” alisema.

Aliyataja mashtaka yaliyomtia hatiani kuwa ni kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha kifungu 70 (1) (2) B cha Sheria ya Wanyamapori na ya Uhujumu Uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambayo hukumu yake ni kwenda jela miaka 25.

Shtaka jingine ni la kula njama ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano jela na shtaka la kupakia shehena katika bandari bubu ambalo adhabu yake ni kulipa faini ya Dola5,000 za Marekani (wastani wa Sh10.5 milioni) na la nne ni kusafirisha nyara za Serikali ambalo adhabu yake ni faini ya Sh50,000 au kifungo cha miaka mitano.

“Kutokana na mashtaka haya, nakupa adhabu ya jumla ya kutumikia kifungo cha miaka 25 jela pamoja na kulipa faini ya Sh3,751,750,000,” alisema Hakimu Kisongo wakati akitoa hukumu hiyo.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Saraji Iboru akisaidiana na Shosa Naiman kuwa Novemba, 2009 katika Bandari ya Koushug, zilikamatwa kontena mbili zenye majina ya PONU na MEAU zikiwa na meno ya tembo ambayo yalifichwa kwenye maboksi ya katani na maji ya kunywa ya chupa.

Wakili Iboru alidai kuwa meno hayo ya tembo yalipokamatwa ulifanyika uchunguzi na kubainika kuwa yalikuwa yakisafirishwa na Kijangwa kutoka Bandari ya Tanga kupelekwa Manila.

Alidai kuwa baada ya uchunguzi, Kijangwa pamoja na washtakiwa wengine watano walikamatwa na wawili kati yao wanatumikia kifungo tangu mwaka 2014 baada ya kupatikana na hatia.

Wakili huyo wa Serikali alidai kwamba baada ya Kijangwa kuhudhuria mahakamani hapo kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza Desemba 10, 2009 lakini ilipotajwa tena Januari 11, 2010 hakutokea tena hadi juzi alipokamatwa wilayani Lushoto.

Akizungumza baada ya kutakiwa na hakimu kujitetea, mshtakiwa huyo alimuomba kutumia busara kwa kumpunguzia adhabu kwa sababu anategemewa na mke ambaye ni mgonjwa.