Muhas yahadharisha hofu magonjwa ya mlipuko

Muktasari:

  • Baada ya matukio kadhaa ya kuhara Muhas imeanza kampeni maalumu inayosisitiza usafi kama njia ya kujikinga na kupambana na magonjwa ya mlipuko.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na minong’ono ya uwepo wa ugonjwa wa kipindupindu katika baadhi ya maeneo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang'una amesema hakuna mgonjwa aliyethibitishwa kuugua maradhi hayo.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Profesa Tumaini Nyamhanga ametoa tahadhari kwa wanafunzi kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kuhara.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 29, 2024, Dk Mang’una amesema mvua zilizonyesha zilitoa tahadhari, hivyo walianza kampeni maalumu inayosisitiza usafi kama njia ya kujikinga na kupambana na magonjwa ya mlipuko.

“Kampeni hii kwa sasa ipo katika maeneo mengi, kuna ukaguzi unafanyika na afua zingine kuhakikisha tunajikinga na ugonjwa huu,” amesema.

Aprili 17, katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam, kuliibuka minong’ono kwamba kuna mtu alifariki dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu na kuzikwa na Jiji.

Hata hivyo, Mwananchi lilipofika eneo hilo kwa ajili ya kuthibitisha, ndugu hawakuwa tayari kuzungumzia hilo.

Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Athumani amesema jambo hilo haliwezi kuzungumzwa kwa kuamini kuwa ni aibu kwa watu wanaowazunguka.

“Hata watu waliokwenda kuzika wamewekwa mbali, hivyo si rahisi kwa ndugu kuzungumzia hili jambo ambalo linaonekana kama fedheha katika familia,” amesema Athumani.

Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Zavery Benela kuzungumzia kuhusu mgonjwa aliyedaiwa kuugua kipindupindu, ameelekeza atafutwe mganga mkuu wa Manispaa ya Konondoni.

“Kuhusu hilo mtafute mganga mkuu wa Manispaa aweze kuliongelea,” amesema Dk Benela.

Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni simu yake iliita bila kupokewa.


Muhas yachukua tahadhari

Hayo yakiendelea, taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi Muhas, Profesa Tumaini Nyamhanga imeeleza kuna mlipuko wa ugonjwa wa kuhara.

“Tulipata taarifa kwamba kuna baadhi ya wanafunzi wameugua kuhara, sasa kutokana na idadi kuwa kubwa ambayo hatukupata namba kamili, kama uongozi wa chuo tukachukua tahadhari ya kuwapatia elimu na namna ya kujikinga,” amesema Profesa Nyamhanga alipozungumza na Mwananchi leo Aprili 29, 2024.

Taarifa hiyo imetoa rai kwa kila mwanafunzi kuchukua hatua za kujikinga, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatumia majisafi yaliyofungwa kwenye chupa kunywa na kupigia mswaki.

“Kama maji ya chupa hayapatikani, tumia maji yaliyochemshwa vizuri na kutunzwa katika hali ya usafi au yaliyotakaswa kwa njia mbalimbali za kuondoa bakteria,” imeeleza taarifa hiyo.

Profesa Nyamhanga amewasisitizia wanafunzi kuhakikisha wanaosha mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka kabla, wakati na baada ya kuandaa chakula.

Pia, kabla na baada ya kuandaa chakula, baada ya kutumia choo na baada ya kumhudumia mgonjwa ambaye ana tatizo la kuhara.

“Kama hakuna uwezekano wa kupata sabuni na maji safi, tumia vitakasa mikono ambavyo angalau vina alkoholi ya zaidi ya asilimia 60,” amesema.

Profesa Nyamhanga amewataka wanafunzi hao kuwa makini na chakula wanachokitumia na kujua mahali kinapoandaliwa.

“Kula chakula kilichopikwa kwa wakati huohuo na ambacho bado cha moto. Epuka vyakula hasa mboga za majani zisizoivishwa na matunda ambayo hayajasafishwa,” amesema.


Chalamila aja na usafi

Aprili 18, 2024 akiwa katika ziara ya kikazi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alitoa maagizo kwa wakuu wa wilaya kukutana na watendaji wa kata kuorodhesha maeneo yenye taka.

Chalamila alisema ni aibu Dar es Salaam kushambuliwa na kipindupindu na badala yake kikasikike katika maeneo ambayo watu hawajastarabika.

“Mahali popote tukisikia kuna kipindupindu tunaanza na mtendaji wa mtaa, mwenyekiti wa mtaa, ofisa afya wa kata kwamba kwa nini umeruhusu kipindupindu kiwepo na unalipwa mshahara, wameshindwaje kusafisha,” alionya.