Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahofu magonjwa ya mlipuko, maji taka yakisambaa mitaani

Maji yakiririka kutoka kwenye chemba ya mfumo wa maji taka yanayolalamikiwa na wananchi mtaa wa mianzini Kata ya Mabatini jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Kutokana na kutitirika kwa majitaka yenye harufu ya kinyesi jijini Mbeya, baadhi ya wananchi wametaka hatua zichukuliwe haraka ili kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko.

Mbeya. Wananchi wa kata za Mbalizi Road na Mabatini jijini hapa wamesema wako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu kufuatia mifumo ya maji taka kutiririsha maji machafu yenye harufu ya kinyesi.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Jumamosi Januari 6, 2024 wamesema hali ni mbaya, kwani uchafu unaotiririka unasababisha mazalia ya wadudu kama nzi na funza na wakati mwingine kuingia mto Meta.

Susan Sangasi mkazi wa mtaa wa mianzini Kata ya Mabatini, amesema hali ni mbaya na msimu huu wa mvua kuna uwezekano mkubwa kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

“Uchafu huo unatilikia kwenye makazi ya watu na kwenye maji ya mto ambao ni tegemezi kwa wananchi kutumia kwa kufulia, kumwagilia bustani za mbogamboga na hata watoto kugelea.

“Mwezi uliopita watoto waliugua ugonjwa wa matumbo ya kuhara na huenda sababu kubwa ikawa ni kunywa maji machafu wanapokuwa wakiogelea, tunaomba wahusika watafute mbadala wa kumaliza tatizo hilo,” amesema.

Naye Neema Mulungu amesema kutokana na hali ilivyo wanaomba Serikali kutambua ukiibuka ugonjwa wa kipindupindu watatumia gharama kubwa ya kutibu na kuua vijidudu vinavyozalishwa kutokana na kinyesi.

“Ufike wakati mifumo ya maji taka ifungwe kulingana na idadi ya watu na sio kuangalia maslahi ya kipato badala ya maslahi ya afya za Watanzania,” amesema.

.

Akizungumza na Mwananchi Diwani wa Kata ya Mbalizi Road, Adam Simbaya amesema kuwa suala hilo limekuwa na usugu, kwani amefuatilia kwenye ofisi za Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa (Mbeya -Uwwas) bila mafanikio.

“Nimefuatilia mara kadhaa  wanafika kuzibua baada ya muda chemba zinatiririsha uchafu na mbaya zaidi ziko kwenye makazi ya watu na watoto wadogo wanachezea na kuwa katika hatari kubwa,” amesema.

Simbaya ameongeza kuwa katika ufuatiliaji alishauri wabadili mifumo ya mabomba ili kuepuka changamoto za kila wakati ambapo alidai kuwa alijibiwa kuwa mamlaka haina bajeti kwa sasa  jambo ambalo limemshtua .

Mwananchi lilipomtafuta Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Neema Stanton kuzungumzia suala hilo simu yake iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.