Biashara ya kaboni yagusa robo ya hekta nchini

Dar es Salaam. Biashara ya hewa kaboni imeanza kueleweka miongoni mwa jamii, ambapo vijiji 100 nchini vinaendelea kunufaika na mapato yatokanayo na biashara hiyo.

Mwananchi limefahamishwa kuwa robo ya hekta za misitu yote nchini imegusa uwekezaji wa miradi inayohusisha biashara ya kaboni kati ya mwaka 2007 hadi mwaka huu.

Biashara hiyo licha ya kuwaingizia watu vipato inazalisha hewa safi kwa ajili ya kufyonza hewa chafu duniani.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu biashara ya Kaboni (NCMC), Profesa Eliakimu Zahabu amesema miradi 22 inawekezwa katika wastani wa hekta milioni 12 kati ya hekta milioni 48.1 zilizopo nchini.

Amesema tafsiri yake ni kuwa eneo lililowekezwa ni asilimia 25 ya eneo lote lenye fursa ya biashara hiyo kwa upande wa sekta ya misitu.

Amebainisha kuwa zaidi ya vijiji 100 vilivyoingia mikataba ya biashara hiyo, vimeonyesha mabadiliko makubwa ya ukuaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.

Miradi hiyo 22 ni sehemu ya miradi 33 inayohusisha uwekezaji chini ya kampuni zaidi ya 20 zinazozalisha na kuuza kwa kampuni zinazotambuliwa kimataifa.

Miradi ya kaboni inahusisha sekta ya nishati jadidifu, taka, majitaka, viwanda, bahari na misitu.

Hata hivyo, Profesa Zahabu amesema kituo hicho hakijafanya uchambuzi wa thamani ya miradi yote iliyowekezwa pamoja na kiwango cha tani zitakazozalishwa kwa ajili ya kufidia uzalishaji wa kaboni katika kipindi cha utekelezaji ambacho ni miaka 30.

“Hadi Juni mwakani tutakuwa tumekamilisha ripoti ya kujua mchango wa miradi yote ikiwamo hii ya biashara ya kaboni, ile ya utunzaji wa hifadhi za wanyamapori na miradi mitatu tuliyoahidi kupitia sekta ya usafirishaji na nishati,  tunataka tujue tani ngapi za kaboni tumeziondoa angani kupitia miradi hiyo,” amesema.

Kwa mujibu wa Mpango wa Soko la Kaboni Afrika (ACMI), mauzo ya tani moja ya hewa chafu iliyofyonzwa na hewa safi kupitia miradi hiyo ni wastani wa Dola 10 (Sh25,000) katika soko huria.

Kwa mujibu wa ripoti ya AMCI iliyotolewa mwaka jana, uzalishaji wa kaboni Afrika unakadiriwa kufikia wastani wa tani bilioni 1.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.

Katika kipindi hicho pia, Afrika inatarajiwa kuanza kuingiza wastani wa mapato ya Dola bilioni 120 (Sh300 trilioni) pamoja na wastani wa ajira milioni 110.


Miradi inayoendelea

Kwa mujibu wa NCMC, kuna miradi mitatu mikubwa inayoendelea katika vijiji mbalimbali nchini iliyoanza miaka ya 2007/08 na inatekelezwa kwa miaka 30 ikiwamo mradi mpya ulioanza 2023/24.

Tayari kuna zaidi ya wanakijiji 26,000 wanaonufaika na Sh4.7 bilioni kila mwaka kupitia kikundi cha Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (WMA) cha Makame. Wanahusisha vijiji vitano vya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara (Kijiji cha Ngabolo, Ndedo, Makame, Katikati na Irkiushiobor).

“Tulisaini na Tanzania Carbon mwaka 2017 mkataba wa miaka 30. Kwa misimu mitatu 2019/22 tumepata mapato ya Sh3.7 bilioni kupitia uvunaji wa tani 510,000 za kaboni katika eneo la kilomita za mraba 1,050, ambazo ni asilimia 27 tu ya eneo lote la hifadhi hiyo,” alisema Meneja wa mradi, Supuk Olekao.

“Tayari mradi umesaidia huduma za afya kwa asilimia 40, maji asilimia 30, elimu zaidi ya asilimia 50 na kusomesha kila anayefaulu kwenda chuo ngazi ya cheti hadi chuo kikuu bure, tumekopesha Sh25 milioni vikundi vitano vikubwa vya akina mama. Bado tunasubiri manufaa miaka 27 ijayo katika mkataba huu,” amesema.

Amesema kuanzia mwaka 2018, wakazi 34,242 katika vijiji vinane vya Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi wanaendelea kunufaika na Sh4 bilioni zilizotokana na mauzo ya hewa hiyo safi kufidia kaboni. Vijiji hivyo ni Lugonesi, Mwese, Lwega, Bujombe, Kapanga, Katuma, Mpembe na Kagunga.

Mradi huo unaendeshwa na halmashauri, taasisi ya Carbon Tanzania kwa kushirikiana na mradi wa tuungane kwa afya na mazingira bora wilayani humo.

Taifa linalazimika kutekeleza miradi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), Itifaki ya Kyoto 1997, Makubaliano ya Paris 2015, yanayoshawishi kupunguza uzalishaji wa kaboni chini ya nyuzi joto 1.5C bila kuathiri ukuaji wa shughuli za kiuchumi.


Biashara, matokeo

Ili wamiliki wa miradi kuuza kiwango cha tani ya hewa iliyofyonzwa katika soko huria, hulazimika kushirikisha kampuni za ushauri zinazohakiki kiwango halisi cha kaboni kilichofyonzwa kabla ya kupatiwa cheti cha ubora na kampuni nyingine kama Verra, Gold Standard, Plan Vivo, ISCC ili kutambuliwa sokoni.

“Wanunuzi ni kampuni binafsi zinazozalisha kaboni zikiwamo  za ndege, madini, gesi, mafuta, viwanda vya saruji, makaa na vifaa vya kielekroniki ili kuchagia juhudi za kuepuka mabadiliko ya tabianchi,”amesema Cosmas Tungaraza, meneja uendeshaji Kampuni ya ADAP.

Yves Hausser ambaye ni mdau wa sekta hiyo na mkuu wa kitengo cha oparesheni katika Kampuni ya ADAP amesema:

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Kitaifa wa Biashara ya Kaboni wa Mwaka 2022, muombaji wa kutekeleza miradi hiyo anapaswa kuwasilisha wazo na andiko la mradi, kulipia usajili, kuandaa tena andiko la mradi kwa viwango vya kimataifa kabla ya kupitishwa na kuanza utekelezaji.


Mahitaji ya soko

Ripoti ya Uwekezaji wa Biashara ya Kaboni Duniani ya mwaka 2023 chini ya Trove Research inaonyesha uwekezaji katika miradi kati ya 2012/2022 ulifikia Dola 36 bilioni (Sh90trilioni) huku nusu ya uwekezaji huo ukifanyika miaka mitatu iliyopita.

Zaidi ya Dola 3 bilioni (Sh7.5 trilioni) zinatarajia kuwekezwa siku zijazo.

Matokeo hayo ya utafiti yanaonyesha kwa sasa uwekezaji wa miradi hiyo ni theruthi moja tu ya mahitaji ya dunia hadi mwaka 2030 ili kufikia malengo ya kupunguza zaidi uzalishaji wa gesijoto chini ya 1.5C. Dunia inahitaji mtaji wa Dola 90 bilioni (Sh225 trilioni) ili kufikia malengo hayo ya mwaka 2030.