Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muwsa kutumia Sh28 bilioni utekelezaji miradi saba ya maji

Muktasari:

  • Uzalishaji wa maji kwa sasa katika mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Moshi (Muwsa) ni wastani wa mita za ujazo 43,322 kwa siku, huku mahitaji halisi yakiwa ni mita za ujazo 71,392 kwa siku.

Moshi. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) inatarajia kutumia zaidi ya Sh28.199 bilioni, kutekeleza miradi saba ya maji safi, lengo likiwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo katika kata 39 inayozihudumia.

 Mbali na miradi ya majisafi, pia mamlaka hiyo itatumia Sh13.5 bilioni kutekeleza miradi mitatu ya upanuzi wa mtandao wa majitaka katika Mji wa Moshi, ili kuboresha huduma hiyo na kupunguza changamoto zilizopo kwa sasa.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Innocent Lugodisha wakati akitoa taarifa kwa Madiwani wa Manispaa ya Moshi, walipotembelea baadhi ya vyanzo na miradi inayotekelezwa kwa sasa, ambapo amesema miradi yote 10, itagharimu zaidi ya Sh41.69 bilioni.

Lugodisha amesema uzalishaji wa maji kwa sasa ni wastani wa mita za ujazo 43,322 kwa siku, huku mahitaji halisi yakiwa ni mita za ujazo 71,392 kwa siku, hivyo ukamilishaji wa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji wa huduma hiyo.

"Hali ya huduma ya majisafi imewafikia wananchi wa Mji wa Moshi kwa asilimia 100, wakati eneo la nje ya manispaa katika Kata 18, hali ya utoaji wa huduma ikiwa ni ailimia 82, lakini kwa upande wa huduma ya majitaka katika Manispaa ya Moshi, imewafikia wananchi kwa asilimia 19," amesema Lugodisha na kuongeza kuwa…

"Kutokana na hali hiyo ya uzalishaji wa majisafi na mtandao wa majitaka, katika mwaka wa fedha 2023/2024,Muwsa imejipanga kutekeleza miradi 10 kwa gharama ya Sh41.69 bilioni, ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi."

Ametaja miradi itakayotekelezwa kuwa ni pamoja na mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi kilometa 84 katika eneo la Manispaa ya Moshi, upanuzi wa mtandao wa majisafi kwa kilometa 131 na ujenzi wa vyanzo vipya vya maji katika Kata 18 za Wilaya ya Hai na Moshi, pamoja na ujenzi wa mradi wa maji Karanga Darajani utakaozalisha mita za ujazo 3,456 kwa siku.

Miradi mingine ni ujenzi wa chujio la maji katika chanzo cha Mang'ana, kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na kuchimba kisima kirefu eneo la mwika, ujenzi wa chanzo cha maji Njoro ya Dobi, tanki pamoja na bomba la kusafirisha maji na mradi wa kuboresha hali ya huduma Shabaha, Sambarai na Mweka Sungu.

Akizungumzia miradi ya majitaka, Lugodisha amesema wanatarajia kufanya upanuzi wa mabwawa ya majitaka kufikia uwezo wa kupokea na kusafisha mita za ujazo 16,000 kwa siku, upanuzi wa mtandao wa majitaka kwa urefu wa kilometa 8.7 na ujenzi wa bomba la majitaka lenye urefu wa kilometa 8.2, kuunganisha kiwanda cha ngozi kilimanjaro, kwenye mtandao huo.

Lugodusha amesema pamoja na mikakati hiyo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wananchi katika kata 12 za Wilaya ya Moshi, kutokuwa tayari kufungiwa mita, hivyo kusababisha ongezeko la maji yanayopotea.

"Upotevu wa maji kwa sasa ni wastani wa asilimia 23, na upotevu huu unatokana na kushuka kwa ufanisi wa baadhi ya mita hasa zenye umri mkubwa, mivujo kwenye baadhi ya bomba za muda mrefu, wizi wa maji pamoja na baadhi ya wananchi wa kata 12 Wilaya ya Moshi kutumia maji bila kuwa na mita," amesema Lugodisha.

Aidha amesema changamoto nyingine ni wizi wa mita na uharibifu wa miundombinu mingine ya maji, ambapo amewaomba Madiwani kusaidia kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kulinda na kutunza miundombinu hiyo na kuiwezesha kuwa endelevu.

Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo ameipongeza Muwsa kwa jitihada wanazofanya katika kuhakikisha wanaendelea kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji na kuwezesha wananchi kupata huduma bora ya majisafi.

Amesema zipo changamoto chache ambazo bado zinaikabili mamlaka hiyo, ambapo wanaendelea kuzishughulikia kwa kushirikiana kwa karibu ili kuweza kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi.

"Mamlaka yetu ni miongoni mwa mamlaka bora za maji nchini na upatikanaji wa maji ni kwa kiwango cha juu, tatizo kubwa ambalo tunapambana nalo kwa sasa ni kuongeza mtandao wa majitaka ambao kwa sasa uko chini ya asilimia 30, na tunahitaji kufikia asilimia 100."

Ameongeza kuwa, "Muwsa inafanya vizuri, tunatambua zipo changamoto chache ambazo wanaendelea kuzifanyia kazi, tumezungumzia pia uchakavu wa miundombinu ya majitaka katika kata za katikati ya Mji, wamesema wanaendelea kuboresha miundombinu hiyo... Tuna uhakika tutaendelea kushirikiana kutatua changamoto zilizopo na kuboresha upatikanaji wa huduma katika eneo letu."

Naibu Meya wa Manispaa ya Moshi, Stuart Nkinda amesema licha ya kwamba Mamlaka hiyo inafanya vizuri katika utoaji wa huduma, zipo baadhi ya changamoto ikiwemo za upungufu wa maji katika kipindi cha kiangazi, changamoto ambayo inaendelea kutafutiwa ufumbuzi kwa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa.

"Ni siku nzuri kwa Madiwani wa Manispaa ya Moshi, kukutana na Muwsa na kuweza kufanya ziara kutembelea miradi, tumeweza kufahamu mikakati ya mamlaka katika kuboresha upatikanaji wa huduma, lakini pia tumeelezwa changamoto zilizopo ikiwemo za wizi na uharibifu wa miundombinu, sisi kama wawakilishi wa wananchi, tunakwenda kushirikiana nao kutoa elimu ili kudhibiti changamoto hizi," amesema Nkinda.